Neema kwa wagonjwa wa saratani

Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan imezindua kituo cha matibabu ya saratani chenye hadhi ya kimataifa (CCC), kitakachotoa huduma kwa wagonjwa wa hospitali hiyo na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kilichogharimu Sh29.9 bilioni.

Saratani inazidi kukua nchini, huku takwimu zikionyesha wagonjwa wapya 40,000 hugundulika, huku 27,000 wakifariki kwa saratani kila mwaka.

Hata hivyo, asilimia 80 ya wagonjwa wanaogundulika hufika katika hatua ya tatu na nne ya ugonjwa, ambayo matibabu yake huwa magumu ikilinganishwa na wanaogundulika katika za mwanzo.

Kituo hicho kinajumuisha huduma za kulaza wagonjwa 100 kwa siku, huku 50 wakipatiwa huduma za mionzi za mashine, 25 kwa matibabu ya tiba kemikali na 25 uchunguzi na huduma za chanjo.

CCC itasaidia kupunguza foleni ya wagonjwa waliosubiri huduma ya tiba mionzi kwa zaidi ya mwezi Ocean Road iliyopo takribani umbali wa kilomita 1.2, kwa wale wanaotumia bima, wanaolipia na wagonjwa wanaotibiwa kwa msamaha watapata matibabu yao Aga Khan pale itakapohitajika.

Miongoni mwa mashine za mionzi za kisasa ni pamoja na ile inayotoa tiba ya miale ya kielektroniki (SRS).

Ufunguzi wa kituo hicho umefanywa leo Alhamisi Mei 2, 2024  na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na unaangazia enzi mpya ya vita dhidi ya saratani nchini, ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akielezea huduma itakavyokuwa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe amesema wagonjwa watakaopata huduma katika kituo cha CCC ni wale wa bima, wanaolipia na wananchi wasio na uwezo.

“Aga Khan watazingatia miongozo ya Serikali, wale wa msamaha kuna utaratibu wa msamaha wa asilimia 100, 5 au 10 kulingana na hali ya kiuchumi ya mgonjwa husika,” amesema.

Hata hivyo, amesema kituo hicho pia kitajikita kwenye kukinga na kwamba bado Serikali ina kazi kubwa ya kuongeza wataalamu katika huduma za saratani na kutambua hatua za mwanzo za saratani hasa ya mlango wa kizazi na matiti zinazoongoza nchini.

Mkurugenzi wa huduma za saratani Aga Khan, Dk Harrison Chuwa amesema kituo hicho kimejengwa kwa Sh29.9 bilioni ikiwa ni sehemu ya Sh35 bilioni za Mradi wa Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) wa miaka mitano.

Amesema kituo hicho kitapunguza idadi ya watu wanaohitaji kwenda kupata matibabu nje ya nchi na kitatoa tiba mionzi, hivyo kitapunguza mzigo kwa Ocean Road kwa kuwa kitafanyakazi kwa ushirikiano na Serikali.

“Tangu kuanza kwa mradi huu, tulianza pamoja na Serikali, Wizara ya Afya walitupa miongozo na sera; na tumesaini makubaliano kati yetu na Ocean Road na Bugando mashine yetu ikiharibika tutapeleka wagonjwa wetu huko kwa matibabu, zikiharibika wataletwa hapa,” amesema.

Akizungumzia mradi wa TCCP amesema kwa miaka minne umeleta manufaa ikiwamo wahudumu 464 wa afya wamepewa mafunzo kuhusu huduma za saratani, watumishi 400 ngazi ya jamii wamepata mafunzo, zaidi ya wananchi milioni 4.5 wamepewa elimu kuhusu saratani.

Amesema zaidi ya watu 700,000 wamepimwa saratani, zaidi ya wagonjwa wapya 39,093 wamegunduliwa kuwa na saratani na hadi sasa, uwasilishaji wa mapema wa wagonjwa wa saratani umeongezeka kutoka asilimia 15 (mwaka 2020) hadi asilimia 31.3 mwaka 2023.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Sisawo Konteh amesema:“Tutaendelea kufanya kazi na Serikali katika kuhakikisha huduma za saratani zenye ubora zinakuwepo nchini, tunahitaji Tanzania iwe kitovu cha matibabu bora na utalii wa matibabu ya saratani barani Afrika.”

Rais wa Taasisi mshirika wa mafunzo ya kiufundi ya Curie, Dk Thierry Philip amesema walitoa ufadhili wa mafunzo ya wataalamu kupitia kituo kikuu cha saratani nchini Ufaransa kama sehemu ya mradi huo mtambuka wa saratani Tanzania TCCP.

Katika ufunguzi huo, Dk Biteko amesema Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika kutoa huduma za afya, hususan magonjwa yasiyoambukiza, hivyo uamuzi wa kujenga kituo cha matibabu ya ugonjwa wa saratani ni kielelezo cha jitihada na mchango kwa nchi.

“Sina shaka ubora wa kituo hiki kilichogharimu bilioni 29.9 bilioni kitakuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa 100 kwa siku katika matibabu ya mionzi na kemotherapia. Kwako Mwana Mfalme Zahra Aga Khan, tufikishie salamu kwa Mtukufu Aga Khan kwamba juhudi zake katika kuhakikisha anaboresha huduma za afya nchini Tanzania zinaonekana,” amesema Dk Biteko.

Amesema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza linaumiza Serikali na familia inaingia hasara kubwa kutibu magonjwa hayo, kuwa na Taifa la watu wenye matatizo ya afya uchumi wake hauwezi kufikiwa.

“Saratani imeathiri watu wa rika tofauti, takwimu za utafiti wa saratani na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha watu milioni 19.3 kote duniani wanagundulika kati yao milioni 10 hufariki kila mwaka.

“Juhudi za kupambana na saratani zinaendelea tulibuni mradi shirikishi mtambuka wa saratani Tanzania uliogharimu Sh35 bilioni na miaka minne ya mradi huu mafanikio kadhaa yamepatikana,” amesema Dk Biteko.

Mwana Mfalme, Waziri Ummy

Mwenyekiti wa kamati tendaji ya Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan, Mwana Mfalme  Zahra Aga Khan amesema uwekezaji uliofanyika utasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi kwa kuwa teknolojia zilizowekwa ni za kisasa zinazoruhusu kutoa tiba kwa wagonjwa waliofikia hatua za juu za saratani.

“Teknolojia tiba inazidi kukua nchini Tanzania, nilipozuru hapa mwaka 1998 kwa mara ya kwanza nikiwa na baba yangu, niliona bado huduma za matibabu zilikuwa nyuma, ni furaha kwangu leo ninavyoshuhudia maendeleo haya na katika utoaji wa tiba, vipimo na wataalamu bingwa ni hatua nzuri na ya kujivunia, nawapongeza timu ya Aga Khan na Serikali,” amesema Mwana Mfalme Zahra.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema: “Kila mwaka Watanzania 40,000 wanagundulika na saratani huku 27,000 wakipoteza maisha na saratani inayoongoza ni ya shingo ya kizazi inayochukua asilimia 23.5 ya saratani zote.”

Amesema Septemba mwaka jana Serikali ilizindua ripoti iliyochapishwa Mei 2022 inaonyesha hali ya ugonjwa wa saratani katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara iliyoonyesha vifo vitaongezeka mara mbili zaidi ifikapo mwaka 2030 kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

“Tuna vifo 520,000 nchi za SADC kwa sasa, vitaongezeka kufikia milioni moja  ifikapo mwaka 2030, juhudi mbalimbali zimefanywa na wadau kutuwezesha miundombinu, kusomesha wataalamu bingwa na bobezi 10, bingwa wa saratani 32 walioenda nje ya nchi, wauguzi 10.

“Bado tuna changamoto ya wataalamu hasa ‘clinical phiysist’ hatuna hawa wataalamu, Aga Khan mnaye mmoja kutoka Bangladesh. Madaktari bingwa wa saratani tunao 35 pekee kati ya 160 wanaohitajika,” amesema Ummy Mwalimu akiahidi ushirikiano na Aga Khan.

Related Posts