Diarra aweka rekodi Afrika | Mwanaspoti

KIPA wa Yanga, Djigui Diarra, ameingia anga za makipa bora Afrika akila sahani moja na Sipho Chaine wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa kucheza mechi nne za hatua ya awali katika Ligi ya mabingwa Afrika bila kuruhusu bao lolote.

Makipa hao wawili wametumia dakika 360 za mechi nne za raundi ya kwanza na ya pili bila kuruhusu bao, wakiwafunika hadi Ronwen Williams wa Mamelodi Sundowns na Mohamed El Shenawy wa Al Ahly, ambao wametumika katika dakika 180 kupitia mechi mbili kila mmoja bila kuruhsu bao lolote hadi sasa.

Diarra amekuwa nguzo muhimu kwa Yanga, akisaidia timu kufika hatua ya makundi bila kuruhusu goli, jambo linalomweka katika kundi la makipa hao.

Diarra ametumia dakika hizo katika mechi mbili za raundi ya kwanza dhidi ya Vital’O Burundi na Yanga ilishinda jumla ya mabao 10-0 ikianza kwa kushinda 4-0 na ziliporudiana ilishinda tena 6-0, kisha ikacheza mechi za raundi ya pili dhidi ya CBE SA ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 7-0.

Diarra aliendeleza umwamba kwa kuisaidia Yanga kushinda 1-0 ugenini jijini Addis Ababa, Ethiopia kisha wikiendi iliyopita ikicheza Uwanja wa Amaan Zanzibar, Yanga ilishinda tena 6-0 na kufanya kipa huyo na Yanga kwa jumla kucheza mechi nne na kufunga jumla ya mabao 17-0.

Rekodi hizo za Diarra zinaenda sambamba na za kipa wa Orlando, Sipho Chaine ambaye naye alicheza mechi nne, zikiwa mbili za raundi ya kwanza dhidi ya Disciples ya Magadascar na kushinda 4-0, ikianza kwa kutoka suluhu ugenini kisha kushinda nyumbani Afrika Kusini kwa mabao 4-0.

Katika raundi ya pili Sipho aliiongoza tena Orlando kuing’oa Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda ugenini 2-0 na wikiendi iliyopita kutakata tena nyumbani kwa bao 1-0 na kuwa miongoni mwa timu 16 zilizotinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Makipa Ronwen Williams wa Mamelodi Sundowns na Mohamed El Shenawy wa Al Ahly nao wakafanya yao katika mechi mechi za raundi ya pili za michuano hiyo ambazo timu zao zilianzia kwa kuzivusha kuingia makundi bila kuruhusu bao, Msauzi akiwa ameisaidia Masandawana kutinga kwa ushindi wa 8-0.

Mamelodi iliikandika Mbabane Swallows wa Eswatini kwa mabao 4-0 ugenini na kurudia tena ushindi kama huo nyumbani, huku El Shanawy yeye aliiongoza watetezi hao wa michuano hiyo, Al Ahly kuopata ushindi wa 3-0 ugenini na nyumbani kushinda pia kama hivyo dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Makipa wengine wa waliofanya vizuri ni Brudel Efonge Liyongo wa AS Maniema Union, ambaye hakuruhusu bao katika mechi tatu kati ya nne aliyocheza na Olorunleke Ojo wa Al Merrikh, ambaye amefungwa mabao mawili tu katika mechi za kufuzu.

Makipa hawa wote wameonyesha kiwango cha juu, lakini Diarra amejitokeza zaidi kutokana na kucheza dakika nyingi zaidi bila kuruhusu bao, huku Olorunleke Ojo kutoka Sudan, pia ameonyesha kiwango kikubwa kwa kuto ruhusu bao katika mechi tatu kati ya nne za raundi za awali.

Wengine waliofanya vizuri ni pamoja na A. Ramdane wa MC Alger, ambaye ameruhusu bao moja tu katika mechi nne na T. Moussaoui wa US Monastir, ambaye alifungwa mabao mawili katika mechi za marudiano lakini bado alionyesha kiwango kizuri katika hatua za awali.

Mchango wa makipa hawa unaonyesha kuwa Ligi ya Mabingwa Afrika imekuwa na ushindani mkali wa makipa bora kutoka sehemu mbalimbali za bara hili.

Msimu uliopita, Diarra alitajwa kuwa mmoja wa makipa bora kutokana na mchango wake mkubwa kwa Yanga, hasa walipofika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Diarra alisema; “Sio rahisi na wala haikuwa uwezo wangu binafsi. Huu ni ushindi wa timu nzima. Tumekuwa na malengo ya kufanya vizuri katika mashindano yote, ndani na kimataifa, na tunaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana.”

Diarra alisifu ushirikiano mzuri kati ya safu ya ushambuliaji na ulinzi, akisema kwamba maelewano ya timu nzima yamekuwa chachu ya mafanikio hayo.

“Najivunia ubora uliopo ndani ya Yanga. Hii sio sifa yangu pekee, ni mafanikio ya timu nzima kwa kuwa tumeshirikiana vizuri kuanzia safu ya ushambuliaji hadi ulinzi,”  aliongeza kipa huyo, aliyetoa sifa kwa mabeki Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’, akisema mchango wao umekuwa mkubwa.

“Job na Bacca wamekuwa muhimu sana, sio tu kwa kuwa mabeki imara bali pia kwa mawasiliano yao uwanjani. Wanatoa sauti kali na maelekezo ambayo yamekuwa msaada mkubwa kwangu,” alisema Diarra.

Diarra anaamini ubora wa kikosi cha Yanga unampa nguvu zaidi uwanjani. Anasema kazi nzuri ya safu ya ulinzi imekuwa ni siri ya mafanikio ya timu katika kutoruhusu bao. Hii inampa nafasi ya kujenga ujasiri na kuendelea kuwa kipa tegemeo kwa timu yake.

Kwa upande mwingine, Diarra alikiri bado wana kazi kubwa mbele yao, akisema;

“Huu ni mwanzo mzuri, lakini safari bado ni ndefu. Tunahitaji kuendelea kujipanga na kuboresha maeneo mbalimbali ya timu ili tuweze kufika mbali kwenye mashindano haya.” 

Related Posts