Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameonya matumizi ya fedha katika chaguzi za ndani ya chama hicho, akiwataka wanachama kuwa makini na fedha alizodai “zimemwagwa kuvuruga uchaguzi huo.”
Lissu pia amesema kuna ugomvi mkubwa katika Kanda ya Nyasa kutokana na uchaguzi wa ndani wa chama hicho, hivyo amewaonya wanachama wa chama hicho kujiepusha nao.
Kauli ya Lissu imekuja wakati Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chadema ikiwa imebatilisha matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Njombe, baada ya kusikiliza rufaa ya mmoja wa wagombea, Ahadi Asajile Mtweve.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa leo Mei 2, 2024, Lissu amesema uchaguzi wa ndani wa chama hicho umetawaliwa na mtafaruku.
“Wakati nakuja hapa Iringa jana na juzi kulikuwa na mtafaruku mkubwa sana, sijui kama mnafahamu, ndani ya chama chetu kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu,” asema Lissu.
Amesema fedha hizo huwa hazipatikani wakati chama hicho kikipambana kufanya mikutano ya hadhara, wala operesheni nyinginezo.
“Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, ninyi mnafikiri hiyo hela ni ya wapi? Mnafikiri hiyo hela ni ya nani? Mnafikiri hiyo hela itatuacha salama? Ukitaka kujua kwamba hatuko salama, fuatilia mitandaoni,” amesema.
Lissu amesema ameamua kuyasema hayo hadharani ili viongozi ambao hakuwataja wayasikie.
“Hizo pesa kwanza sio za Chadema kwa sababu sisi huwa hatuna hela siku zote, kwa hiyo hizi hela ni za nani? Na zinavyosambazwa hivi ni kwa ajili ya manufaa ya chama chetu?”
Huku akibainisha kuwa, kuna watu walimtaka asifike katika kanda hiyo kuzungumza hadi uchaguzi uishe, Lissu amewaonya wanachama wa chama hicho kujiepusha na fedha hizo.
“Niliambiwa nisije kuzungumza kwenye mkutano huu, nisije kabisa, niliambiwa nisubiri uchaguzi upite ndio nije, yaani nisubiri mchafuane na kukatana mapanga na kutukanana na kuraruana, halafu mkishapasuana ndio nije, nikasema nitakuja nizungumze hadharani, nije niwape za usoni.
“Nawaombeni wanachama wa Chadema wa Iringa, muwe macho na hizi pesa, zitatuangamiza tusipoangalia. Sio Iringa peke yake, ni Njombe kila mahali nchi nzima, tusipoangalia zitatuangamiza. Chagueni viongozi ambao mnajua hawa hawatatuuza.
“Kuweni macho na hizo pesa, mkachagueni mnaowaamini, sio wanaowahonga, ndio nimesema, mmenielewa?”
Ameendelea kusisitiza kuwa mara nyingi chama hicho kinakuwa na ukata wa fedha kinapofanya shughuli zake na kushangaa sababu ya kuwepo kwa fedha akati wa uchaguzi, “kwenye uchaguzi zimetoka wapi?”
“Mimi nawaombeni wananchi wa Iringa na wananchi wa Kanda hii, kwa sababu huu ugomvi ni mkubwa sana na wananchi wa kanda nyingine kuweni macho na pesa hizi chafu.
“Watu wanasema pesa ni pesa, hata za Yuda Iskariote ni pesa. Sasa nyie mnataka hela ya Yuda ya Islariote?”
Alipoulizwa kwa simu leo, Katibu wa Kanda ya Nyasa wa chama hicho, Gwamaka Mbughi amesema hawezi kuzungumzia tuhuma hizo, kwa kuwa uchaguzi wa kanda hiyo unasimamiwa ofisi ya Katibu Mkuu.
“Msimamizi wa chaguzi hizi ni katibu mkuu, hivyo siwezi kusema chochote,” amesema.
Katibu Mkuu John Mnyika hakupatikana kwenye simu yake, lakini Naibu Katibu Mkuu (Bara), Benson Kigaila alipoulizwa alisema, hakuwezi kuzungumzia kwa kuwa hajamsikia Lissu.
Katika kanda hiyo, Mbunge wa zamani wa Iringa, Peter Msigwa na mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) wanachuana, ambapo kwa mara ya kwanza wanachama wa kila mgombea wameandamana kwenda kuwachukulia fomu kwa nyakati tofauti.
Walipotafutwa kwa simu kuzungumzia kinachoendelea kwenye uchaguzi huo hawakupokea simu zao.
Awali Lissu ameeleza kutoridhishwa na mabango yenye picha zinazomwonyesha Rais Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi na makada wa Chadema, akiwemo yeye.
Lissu amekwenda mbali akisema atapeleka hoja kwenye Kamati Kuu ya Chadema ili waajadili kumshaki Rais Samia kwa picha hizo kusambazwa nchi nzima.
Miongoni mwa picha hizo ni ile inayoomwonyesha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na baadhi ya viongozi wa Baraza la Wanawake (Bawacha) katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 2023 na nyingine ikimwonyesha Lissu akisalimiana na Rais Samia walipokutana Ubeligiji.
Akizungumza katika mkutano huo, amesema picha hizo Lissu amesema zinatumika kupotosha msimamo wa chama hicho.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amelipoulizwa kuhusu mabango hayo alisema picha hizo zinaonyesha upendo kwa vyama vya upinzani.
“Anaalikwa anahudhuria anakaa nao vikao vya maridhiano, kwa maana hiyo Tanzania ni yetu sote, mtazamo wa kisiasa usifikie hatua ya kuligawa Taifa hili,” amesema Makalla.
Ameongeza, “hakuna kosa lolote la mabango hayo kuwekwa na picha hizo hata kwenye mitandao ya kijamii zipo, watakuwa wanahangaika tu kusema picha hizi hawazitaki lakini zipo na historia imeshatengenezwa na alienda kwenye mkutano alioalikwa na kuonyesha mfano wa uongozi.”
Kabla ya mkutano wa hadhara, Lissu aliyeongozana na viongozi wengine wa chama hicho, akiwamo mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche walishiriki maandamano mitaani.