Dar es Salaam. Wanaume nchini wameshauri kutumia njia ya kisasa ya uzazi wa mpango ya kufunga mirija inayopitisha mbegu za kiume, kwenda kukutana na yai la mwanamke ili kutoa fursa ya kulea watoto waliowazaa kwa kuwapa mahitaji yanayotakiwa.
Imeelezwa kutokufanya hivyo kwa kundi hilo na kuwaachia wanawake pekee, wakati mwingine ni chanzo cha kuendelea kuzaa watoto bila mpangilio na kushindwa kuzingatia malengo waliyojiwekea kama familia.
Akizungumza Dar es Salaam wakati anatoa elimu na huduma kwa wananchi wa Tandika wilayani Temeke, Mshauri Mwandamizi wa uzazi wa mpango kupitia miradi ya USAID ya Afya ya mama na mtoto (MCH), Dk Gloria Shirima amesema watatumia wiki ya uzazi wa mpango kuongea na vijana waelewe njia hiyo.
“Tunataka wajue kinachofungwa ni mirija inayopitisha mbegu za kiume kwenda kukutana na yai la mwanamke, kwenda kutengeneza mtoto lakini nguvu za kiume haziathiriki,” amesema Dk Shirima.
Dk Shirima amesema kuhusisha imani potofu na njia za uzazi wa mpango katika jamii mbalimbali nchini ni sababu ya mkwamo kwa wengi kutumia.
“Tunajipanga kuongeza utoaji elimu ya matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango, watu waelewe ili waondokane na imani hizo potofu,” amesema.
Amesema waliowengi wamekosa ufahamu na kujua njia huku akieleza malengo yao kina mama na baba wajue njia za uzazi wa mpango za kisasa wanaweza kutumia kwa muda gani na wajue maudhi madogomadogo.
“Tunatamani kuongeza ufahamu kwakuwa hiyo ni changamoto zaidi kuna wanaoamini ukitumia uzazi wa mpango unapata saratani, baadhi wanasema watakuwa wagumba na hawawezi kupata watoto tena,” amesema.
Shirima ameeleza faida za uzazi wa mpango inamsaidia mama kulinda afya yake na ya mtoto wake aliyezaliwa na kuisaidia familia kupanga idadi ya watoto wa kuzaa kwa kipindi fulani.
“Kitaalamu walau mtoto hadi mtoto wapishane miezi 24 katika kuzaliwa na hali hiyo inatoa fursa kwa wazazi kuhudumia watoto wao kwa wakati na kugharamia mipango ya shule,” amesema.
Muuguzi wa huduma za mama na mtoto katoka kituo cha afya cha Alafa Tandika, Latifa Masasi amesema tangu wameanza kutoa elimu hiyo, watu 260 wamenufaika.
“Kati ya hao akina baba wawili wamefunga uzazi, mama mmoja na tumeendelea kwenye vitanzi na sindano na waliopata huduma walikuwa 120,” amesema.
Amesema hamasa ni kubwa hasa kina mama lishe, kulingana na eneo ambalo wanatoa huduma hiyo pamoja na madereva bajaji ni wengi.
“Kina baba walikuwa wengi kuliko kina mama na wamepata elimu na walikuwa na maswali mengi tumewaelewesha na wameelewa inawezekana,” amesema
Mmoja wa washiriki wa elimu hiyo, Katibu wa Baba Bora, Mkoa wa Dar es Salaam, Athuman Omary amewasihi akina baba kuchangamkia njia hiyo.
“Ni muhimu kwa kinababa nao kufunga uzazi wanapohisi wamefikia ukomo kulingana na hali maisha yao. Wengi tulikuwa tunaamini ni akina mama tu wanapaswa kufunga na kinababa tunatumia kondomu basi,” amesema.
Amesema baada ya kupata mafunzo hayo kutoka kwa wataalamu hao, wanaume hata wakifunga uzazi haiwazuii kwa baadaye kutaka kuzaa tena kwani huwa wanafanyiwa upasuaji mdogo wa kuziba njia za mbegu.
“Baada ya muda kama utaona unataka kuzaa unaenda kurudishia tena. Na uwanaume wako unaendelea kama kawaida na tendo utakuwa unafanya kama kawaida,” amesema.
Amesema hicho ni kitu kipya amekipata ataenda kuwa balozi kwa kusambaza elimu kwenye vikundi vyao vya akina Baba bora.
“Wasiwasi ilikuwa tukifanyiwa upasuaji ngoma itakuwa haifanyi tena kazi na biashara ile ikiwa haifanyi kazi huwezi kujihesabu kama mwanaume mkamilifu,” amesema.