HAUKUWA msimu wao. Ndivyo unavyoweza kusema kwa timu kongwe ya Pazi kwenye Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ikiziacha nyingine zikitinga hatua ya nane bora.
Pazi iliyowahi kushiriki mashindano ya Afrika yaliyofanyika Afrika Kusini (BAL) 2023, iliondokewa na baadhi ya nyota wake siku mbili kabla ya kuanza usajili.
Wachezaji walioondoka ni Haji Mbegu, Erick John, Ally Abdallah na Josephat Peter (Dar City), Evance Davies, Mwalimu Heri (UDSM Outsiders) na kuwatumia waliokuwepo Gidibo Tindwa, Denis Chibura, Martin Kolikoli na Robert Tasire hadi mzunguko wa kwanza unamalizika.
Awali Kolikoli aliwahi kuliambia Mwanaspoti, timu yao itakuja kuaa sawa katika usajili utakaofanywa katika mzunguko wa pili na ilibadilika na kuanza kushinda baadhi ya michezo.
Katika mzunguko huo, ilizifunga DB Oratory kwa pointi 80-74, KIUT 82-70, Mgulani (JKT) 62-49, Ukonga Kings 62-48 na Vijana ‘City Bulls 68-55.