Mwalimu mkuu jela miaka 30 kwa kubaka, kumpa mimba mwanafunzi

Misungwi.  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilimo, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Paulo Charles (40) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi wa miaka 16 wa shule hiyo.

Akitoa hukumu hiyo leo Alhamisi Mei 2, 2024, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Misungwi, Amani Shao amesema katika kesi ya jinai namba 79 ya mwaka 2023, Mahakama hiyo pasi na shaka imekubaliana na ushahidi wa upande wa mashitaka uliotolewa na mashahidi wanne wakiongozwa na mwendesha mashtaka wa Polisi Mkaguzi Msaidizi, Ramsoney Salehe.

“Mahakama imekubaliana na ushahidi wa upande wa mashitaka kwa shahidi wa kwanza mwanafunzi aliyeieleza Mahakama kuwa mtuhumiwa alimbaka na kumtishia kwa kisu kwa nyakati tofauti Februari na Machi mwaka jana, ushahidi huo uliungwa mkono na Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Wilaya ya Misungwi, Kanyaga Sospeter aliyeieleza Mahakama kuwa mwanafunzi ameingiliwa na kuwa na ujauzito,” amesema hakimu Shao.

Hakimu huyo baada ya kukubaliana na ushahidi uliotolewa na  upande wa mashitaka ambao alisema haujaacha shaka yoyote, alitamka kuwa anamtia hatiani mshitakiwa.

Hata hivyo, kabla ya kutaja adhabu Hakimu Shao alimtaka mshtakiwa atamke ni kwa nini asipatiwe adhabu kali kutokana na kosa alilolifanya.

Mtuhumiwa ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ukiriguru wilayani Misungwi, alijitetea kuwa hakufanya mapenzi na mwanafunzi, pia anategemewa na wazazi na familia yake.

Mwendesha mashitaka, Ramsoney Salehe aliiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa walimu wengine waliopatiwa dhamana na wazazi ya kuwalea na kuwafundisha watoto lakini wao wanakengeuka na kuwakatiza masomo.

Hivyo, Hakimu Shao akatoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mwalimu huyo.

Juni 27, 2023, Ramsoney alimsomea hati ya mashitaka mwalimu mkuu huyo kuwa kwamba kwa nyakati tofauti kati ya Februari na Machi, alikuwa akifanya mapenzi na mwanafunzi wa miaka 16 wa darasa la saba, kinyume na kifungu 130 (1) 2 (e) na kifungu cha kanuni ya adhabu ya makosa ya jinai 131 sura ya 16 kama ilivyorejewa mwaka 2002.

Pia, alimpa ujauzito mwanafunzi huyo kinyume na sheria ya elimu kifungu cha 60 (A) kifungu kidogo (4) sura 353 kama kilivyolejewa na sheria 2 ya mwaka 2016.

Related Posts