Kanuni, masharti kwa wenye nia ya kugombea uongozi

Dodoma. Wakati mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ukiendelea, kanuni za uchaguzi huo zimeweka masharti yanayotakiwa kuzingatiwa na wagombea wote ikiwamo kuwa wanachama na wadhaminiwa wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 zinalenga kuleta uwazi, haki, na usawa katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Nafasi mbalimbali za uongozi zitakazogombewa zimeainishwa pamoja na masharti yanayopaswa kufuatwa na wagombea.

Kwa mujibu wa kanuni nafasi zitakazogombewa ni muhimu kwa uongozi na utawala wa maeneo husika.

Kanuni hizo zimeainisha aina za nafasi zitakazogombewa, taratibu za uchaguzi kwa kila nafasi, na masharti kwa wagombea.

Mwenyekiti wa kijiji ni kiongozi mkuu wa utawala katika kijiji. Nafasi hii inagombewa katika maeneo yote yaliyoainishwa kama vijiji.

Mwenyekiti wa kijiji anachaguliwa na wananchi wa kijiji husika kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa mwaka 2024.

Wagombea wa nafasi hii wanapaswa kuwa na sifa zinazotambulika kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania na mkazi wa kijiji anachogombea.

Uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 571 la Mwaka 2024).

Hizi ni kanuni zilizotangazwa na Serikali kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa nafasi ya mwenyekiti wa kijiji.

Wajumbe wa halmashauri ya kijiji ni sehemu ya utawala wa kijiji, ambao wanawajibika kusimamia mipango ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za kijiji.

Halmashauri ya kijiji inaundwa na wajumbe kutoka makundi mawili, kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake, na kundi la wanawake pekee. Nafasi hizi zinahakikisha ushiriki wa kijamii na uwakilishi wa watu wa jinsia zote.

Uchaguzi wa wajumbe hawa pia utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 571 la Mwaka 2024).

Wajumbe kundi la wanawake

Hili ni kundi maalumu lililoainishwa kwa ajili ya wanawake pekee, lengo likiwa ni kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na utawala wa kijiji.

Nafasi hii ni muhimu kwa maendeleo ya kijiji, hasa kwa kuimarisha usawa wa kijinsia katika uongozi.

Vitongoji ni vitengo vidogo ndani ya vijiji na miji, na vinasimamiwa na wenyeviti wa vitongoji.

Nafasi hizi zinagombewa na wagombea wanaotaka kushiriki katika kusimamia maendeleo ya vitongoji.

Wenyeviti wa vitongoji wanachaguliwa na wananchi wa vitongoji hivyo kwa mujibu wa kanuni husika za mwaka 2024.

Uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji katika wilaya utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 571 la Mwaka 2024.

Mwenyekiti wa kitongoji ni nafasi ya uongozi katika maeneo ya miji midogo yaliyopewa hadi hiyo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na shughuli za kimaendeleo.

Wagombea wa nafasi hii wanachaguliwa na wakazi wa miji hiyo kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kanuni za uchaguzi wa mwaka 2024.

Kwa nafasi hii, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 572 la Mwaka 2024).

Kanuni hizi zinaweka utaratibu maalumu wa jinsi wagombea watakavyochaguliwa na taratibu za kuendesha kampeni zao.

Hata katika maeneo ya miji, nafasi za mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji (kundi mchanganyiko na kundi la wanawake), na wenyeviti wa vitongoji zinagombewa.

Hii inaonyesha umuhimu wa kushirikisha wananchi katika ngazi za chini hata katika maeneo yaliyoendelea kimaendeleo kama miji.

Uchaguzi wa nafasi hizi utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 573 la Mwaka 2024).

Mwenyekiti wa mtaa ni kiongozi wa mtaa ambaye anasimamia shughuli zote za mtaa, ikiwemo usalama, maendeleo, na ushirikiano kati ya wakazi wa mtaa huo.

Nafasi hii ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa mtaa unakuwa na uongozi thabiti unaowezesha utekelezaji wa sera za maendeleo za mtaa.

Kamati ya mtaa ina wajumbe kutoka kwa kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake, ambapo wajumbe hawa wanashiriki katika maamuzi ya maendeleo na usimamizi wa shughuli mbalimbali za mtaa.

Uchaguzi wa wajumbe hawa utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za mwaka 2024.

Kamati ya mtaa (Kundi la wanawake)

Hili ni kundi maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya wanawake pekee. Lengo kuu la nafasi hii ni kuhakikisha kuwa wanawake wanapata uwakilishi katika ngazi za maamuzi na kushiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo ya mtaa.

Uchaguzi wa nafasi hizi utafanyika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za Mwaka 2024 (Tangazo la Serikali Na. 574 la Mwaka 2024).

Wagombea wa nafasi hizi za uongozi wanatakiwa kutimiza masharti maalumu ili  washiriki uchaguzi yakiwamo mgombea lazima awe raia wa Tanzania mwenye sifa nzuri kisheria, awe na umri wa miaka 18 au zaidi.

Pia, mgombea anatakiwa kuwa mtu mwenye rekodi nzuri ya maadili na asiwe amewahi kupatikana na hatia ya makosa ya jinai, kuwa na  udhamini kutoka kwa wapiga kura wa eneo husika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa tayari ametangaza jumla ya vijiji 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274 kuwa vitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Orodha hiyo imejumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa tangazo la Serikali ambayo pia yalihusisha tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Tangazo hilo limebainisha mipaka ya vijiji, mitaa na vitongoji vitakavyohusika katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na pia limerejesha vijiji vya Ngorongoro vilivyofutwa kwa tangazo la Serikali namba 673 na Tangazo la Serikali namba 674 la Agosti 2, 2024.

Mbali na kuwataka Watanzania kujiorodhesha katika orodha ya wapiga kura kati ya Oktoba 11 hadi Oktoba 20, 2024, pia amewataka kujiandaa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo.

“Ofisi ya Rais Tamisemi imejiandaa vyema kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki katika misingi ya 4R kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameendelea kusisitiza.”

“Mchakato huu ni fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya maeneo yao,” alisema Mchengerwa.

Related Posts