Kiungo Yanga aanika kuhusu namba 17

KIUNGO wa Yanga Princess, Agnes Pallangyo amesema lengo la kutumia jezi namba 17 ni kwa sababu ya kumkubali nyota wa kimataifa, Cristiano Ronaldo.

Nyota huyo alisajiliwa msimu huu akitokea Fountain Gate Princess ya Dodoma ambayo ilimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi ya Wanawake (WPL).

Akizungumza na Mwanaspoti, Pallangyo alisema kwenye maisha yake hatokuja kutumia jezi ya namba yeyote isipokuwa saba ama inayomalizikia na namba hiyo.

Aliongeza kuwa sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na kumpenda Ronaldo ambaye amefanya makubwa duniani hivyo kutumia namba hizo ni sababu ya upendo wake kwake .

“Kila mchezaji anatumia namba na maana yake kwangu mimi ni sababu ya kumkubali Ronaldo ambaye licha ya umri wake mkubwa lakini anafanya vitu vikubwa,” alisema Pallangyo.

Kuhusu ushindani wa namba alisema “Kila mchezaji mazoezini anapambana kuonyesha juhudi zake binafsi ili kupata namba ya kucheza kutokana na ubora wa mchezaji mmoja mmoja.”

Kabla ya kusajiliwa na Yanga alipita timu mbalimbali ikiwemo Majengo Queens  Baobab Queens, Tanzanite, Simba Queens Fountain Gate na sasa Yanga Princess.

Related Posts