Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuchunga kauli zao kwa sababu zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani hasa kipindi hiki taifa likielekea kwenye chaguzi.
Jaji Mutungi amebainisha hayo leo Septemba 26, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi wanawake wa vyama vya siasa kuhusu baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutoa kauli za matusi na kichochezi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Wanawake hao wamewasilisha malalamiko yao wakimtaka Msajili, kama mlezi wa vyama vya siasa nchini, kukemea jambo hilo kwa sababu linaweza kusababisha vurugu zinazoweza kuhatarisha amani.
Akizungumzia malalamiko hayo, Jaji Mutungi amewapongeza wanawake hao kwa kufuata njia sahihi ya kuwasilisha kwake malalamiko yao badala ya kuanza kujibizana na viongozi hao mitandaoni.
“Nimeyapokea malalamiko yenu, nitayafanyia kazi na ofisi yangu ina utaratibu wa kushughulikia mambo haya, kwanza, lazima nipate ushahidi, kisha niwaite hao wanaolalamikiwa, niwaite na nyinyi tena, ndipo nifanye uamuzi.
“Nitumie fursa hii kukemea vitendo vya aina hii (kutoa lugha za kichochezi na matusi) kwa sababu mambo kama haya yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati tukielekea kwenye chaguzi,” amesema.
Awali akiwasilisha malalamiko hayo, mwakilishi wa viongozi wanawake wa vyama vya siasa, Saumu Rashid ambaye pia ni Katibu Mkuu wa UDP, amesema wameamua kupeleka malalamiko hayo kwa Msajili kwa sababu wameamua kubeba amani kama ajenda yao.
Amesema vitendo vya baadhi ya wenzao kwenye vyama vya siasa vinahatarisha amani na usalama wa nchi kwa sababu wanakosa staha na adabu kwa viongozi wa kitaifa kwa kutukana na matusi na kauli nyingine za kichochezi.
“Sisi viongozi wa vyama vya siasa wanawake tumekubali kutekeleza matakwa ya sheria zetu pamoja na Katiba. Majukumu yetu kama vyama vya siasa tunahitaji kusimamiwa na wewe msajili, wewe ndiyo refa kwenye huu mchezo,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Wanawake kutoka chama cha AFP, Zawadi Nayuka baadhi ya wanawake wanaogopa kushiriki kwenye michakato ya kisiasa kwa sababu ya kuogopa kauli zinazotolewa na wanasiasa.
“Sisi tumeleta malalamiko yetu, yeye ataangalia kipi cha kufanya ili kutenda haki. Hatutaki kuona kauli za kichochezi zinatolewa na viongozi wa vyama vya siasa wenye uchu wa madaraka na wasiojali umuhimu wa amani iliyopo,” amesema.