Madumu ya petroli yalivyookoa watu 29 kuzama Ziwa Victoria

Mwanza. Watu 29 wamenusurika kifo baada ya mtumbwi wao kuzama Ziwa Victoria huku wakitaja madumu ya petroli kunusuru maisha yao.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza leo Septemba 26, 2024 na waandishi wa habari amesema boti hiyo imezama saa 11:10 jioni ya jana Jumatano ikitokea Mwalo wa Kirumba jijini humo kwenda kisiwa cha Goziba kilichopo Wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera ikiwa na watu 31, mizigo pamoja na madumu ya petroli 58 yenye ujazo wa lita 270.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa amesema katika ajali hiyo watu 29 walifanikiwa kuokolewa, mtu mmoja amefariki dunia na mwingine hajulikani aliko huku jitihada za kuendelea kumtafuta zikiendelea.

Amesema mtumbwi wenye namba za usajili TMZ 012212 unaomilikiwa na Amoni Lutabanzibwa (MV SEA FALCON) ukiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa 31, nahodha na msaidizi wake uliondoka katika mwalo wa Kirumba kuelekea katika kisiwa cha Goziba ulipofika eneo la Bwiru Wilaya ya Ilemela mtumbwi huo ulipogonga mwamba hali iliyosababisha kupinduka na kuzama ukiwa na watu na mizigo.

“Katika ajali hiyo kwa mujibu wa maelezo ya nahodha na msaidizi wake ulikuwa na abiria 31 ambapo watu 29 wameokolewa wakiwa hai, mmoja amepatikana akiwa amefariki dunia ambaye ametambuliwa kwa jina la Kharidi Rajabu (6), mwanafunzi wa darasa  la kwanza katika Shule ya Msingi Goziba, Wilaya ya Muleba na mtu mwingine ambaye hajulikani jina aliyekuwepo katika ajali hiyo bado tunamtafuta,” amesema Mutafungwa.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa amesema:”Waathirika wa ajali hiyo walikutwa wakiwa wanaelea kwenye maji, huku wakiwa wameshikilia madumu ya mafuta na wengine wakijitahidi kuogelea kwa ajili ya kujiokoa, walifikishwa nchi kavu na kupatiwa huduma ya kwanza kisha walipelekwa hospitali ya Mkoa Sekou-Toure kwa matibabu.”

Wakisimulia leo Septemba 26, 2024 manusura wa ajali hiyo wamesema baada ya kuona mtumbwi umeanza kuzama walilazimika kumwaga mafuta ya petroli kisha kubaki na madumu ambayo walitumia kujiokoa ili wasizame.

Ule mtumbwi baada kuonyesha dalili za kuzama huku maji yakiingia kwa wingi ndani tukawaomba waturudishe lakini wao wakatujibu kwamba tujikaze hali itatulia lakini ghafla mabadiliko yakawa makubwa maji yakajaa hata wao wakashindwa namna ya kufanya baada ya mtumbwi kupasuka,” amesema Lucia Kabagwa mmoja wa wahanga wa tukio hilo.

“Baada ya hapo ndio tukaanza kupiga kelele ya kuomba msaada maana tulikuwa katikati ya maji katika harakati hizo ndo tukapata wazo la kumwaga mafuta ya petroli ili yatusaidie kutuokoa hayo ndio yametuokoa maana tulikuwa tumeshikilia mpaka pale wavuvi wadogo wadogo wenye mitumbwi midogo walipofika na kuanza kutuokoa,” amesema.

Akiunga maelezo hayo Noris Mwene (38) mfanyabiashara wa dagaa kutoka jijini Dar es Salaam amesema baada ya mtumbwi kuanza kuzama aliwapigia simu ndugu na wafanyakazi wenzake akiwaomba wazidi kumwomba Mungu watoke salama katika ajali hiyo.

“Kwenye mtumbwi nilikuwa nimepanda na shemeji yangu, yeye ni mtaalamu wa uvuvi akaniambia chukua dumu moja la mafuta mwaga kisha ulifunike ili likusaidie kujiokoa saizi tumeshazama.

Kweli alivyosema hivyo nikapiga simu kwa ndugu zangu waliopo Dar es Salaam lakini pia nikapiga simu ofisini kwangu Makambako nikawaambia watuombee maana huku tunazama sijamaliza hata kuongea mtumbwi ukawa umezama, shemeji yangu ndio alikuwa wa kwanza kuchukua dumu moja lakini cha kusikikitisha mpaka sasa simuoni,” amesema.

Hata hivyo, Mwene akisimulia namna walivyookolewa na kuibiwa mali zao amesema baada ya kupata ajali hiyo mtumbwi wa kwanza wa wavuvi ulifika katika eneo hilo na kuchukua mabegi na mali zingine kisha kuondoka bila kutoa msaada wowote ambao walikuja kupata kwa wavuvi wadogo wenye mitumbwi midogo.

“Wakati tunapiga kelele za kuomba msaada huku tukiendelea kumwaga mafuta kuna mtumbwi mkubwa mmoja wa wavuvi ulipita katika lile eneo ambacho walifanya walichukua baadhi ya madumu ya mapipa na kukusanya mabegi yetu ambayo yalikuwa na fedha na kuondoka navyo tukabaki tunapiga kelele huku tukiomba Mungu atusaidie huku tukiwa tumeshikilia madumu,” amesema.

“Ajali imetokea kuanzia saa 12:30 jioni, mimi ambaye ndio nilikuwa wa kwanza kuokolewa na mwenzangu nimeokolewa saa 3:30 usiku lakini wengine wameokolewa kuanzia saa 4:30 mpaka saa 5:00 usiku baada ya kuokolewa na wavuvi wa kokoro na kufika nchi kavu nikaanza kuwaomba wavuvi wengine msaada wa kwenda kuwaokoa wengine japokuwa walikuwa wakigoma lakini wachache hasa wavuvi wadogo ndio waliotuokoa,” amesema Mwene.

Hata hivyo, Mwene anasema kwenye ajali hiyo amepoteza Sh8 milioni ambayo ilikuwa kwenye begi kwa ajili ya kwenda kununua dagaa za biashara huku akidai mama mwingine kapoteza Sh11 milioni baada ya kuona begi limekuwa zito.

Wahudumu wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture wakimchunguza mmoja ya waliopata ajali ya mtumbwi iliyotokea Septemba 25 mwaka huu katika Ziwa Victoria.

Kwa upande Jackson Joseph ameiomba Serikali na wasamalia wema wawasaidie kwa hali na mali akidai kwa sasa hawana msaada kutokana na kuibiwa mali na na mavazi baada ya ajali hiyo kutokea.

“Kuna mitumbwi mingine ya mashine ilikuja pale badala ya kuokoa wenyewe wakawa wanakusanya mabegi wanaweka kwenye mitumbwi yao hali ambayo imepelekea mpaka sasa hatuna hata mavazi ya kuvaa kwahiyo tunaomba Serikali na wadau wengine watusaidie,” amesema Joseph.

Wavuvi wasimulia walivyookoa

Mvuvi katika Mwalo wa Butuja Manispaa ya Ilemela mkoani humo, Maiko Magange akisimulia namna walivyookoa amesema baada ya kusikia kelele za watu wakiomba msaada majini walifika katika eneo hilo wakiwa na mtumbwi mdogo na kufanikiwa kuwaokoa watu takribani 10.

“Baada ya kusikia kelele za watoto na watu wakitaka msaada kwa sababu ya udogo wa chombo chetu tulienda eneo la tukio tukaanza kuwaokoa wawili na kuwapeleka nchi kavu mpaka mwisho wa siku tukajikuta tumeokoa kama watu kumi wakatu huo na polisi wakawa wamefika lakini pia wavuvi wengine pia walikuwa wanawaokoa wengine,” amesema Magange.

Mvuvi mwingine ambaye pia alishiriki katika uokoaji, Hashim Hamad amesema kutokana na wavuvi wengi kutokuwa na elimu ya uokoaji walikuwa wakiogopa kwenda kutoa msaada hivyo kuiomba Serikali kuwajengea uwezo wavuvi namna ya kufanya uokozi inapotokea majanga kama hayo.

Akizungumzia hali za majeruhi Mganga mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture, Dk Bahati Msaki amesema baada ya kuwapokea na kuwapatia huduma 14 waliruhusiwa kurudi nyumbani huku 14 wengine wakiendelea na matibabu hospitalini hapo.

“Jana Septemba 25, 2024 muda wa saa 4 usiku tulipokea majeruhi 28 waliotoka kwenye ajali ya boti iliyotokea Ziwa Victoria kati ya hao 22 walikuwa ni wanaume na wanawake sita,” amesema.

“Baada ya kuwapokea na kuwapatia huduma 14 waliruhusiwa walikuwa na maumivu na majeraha madogo madogo lakini 14 tuliwalaza na wapo hodini wanaendelea kupata huduma na hali zao sio mbaya wanaendelea vizuri kati ya hao waliolazwa nane ni wanaume na 6 ni wanawake pia tulipokea maiti ya mtoto mmoja wa kiume ambaye anaitwa, Khalidi Rajabu (6),” amesema Dk Msaki.

Related Posts