Wenye ndugu makaburi ya Ufi Ubungo Maziwa ujumbe wenu huu hapa

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 100 kutoka maeneo mbalimbali wamejitokeza kutambua makaburi ya ndugu zao walizozikwa katika eneo Ufi, Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam.

Makaburi hayo yanahamishwa ili kupisha upanuzi na ujenzi wa barabara ya Ufi (Ubungo Maziwa- Shekilango, inayotakiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Katika eneo hilo makaburi yote yaliyopo karibu na barabara hiyo ambayo idadi yake hadi sasa haijafahamika yanatakiwa kuondolewa kupisha ujenzi huo utakaotekelezwa na Mkandarasi wa China Sichuan Road and Bridge Group Corporation Ltd (SRBG) anayehusika na upanuzi wa Barabara ya Ubungo – Kimara na barabara shikizi za Morogoro na Kawawa.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana Jumatano, Septemba 25, 2025 Mkandarasi SRBG, ametoa siku saba hadi Oktoba 2, 2024 ndugu kujitokeza Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Kisiwani kwa ajili ya utambuzi kabla ya kuhamishwa.

“Kufuatia ujenzi huu kuna baadhi ya makaburi yaliyopo kwenye eneo la ujenzi yanahitajika kuhamishwa ili kupisha ujenzi kwenye barabara hii.

Hivyo basi, tunaomba ndugu wanaohusika na makaburi katika eneo hilo la Makaburi ya UFI mkabala wa barabara ya Shekilango wafike katika ofisi za serikali za mtaa, Mtaa wa Kisiwani, Kata ya Ubungo kuanzia Septemba 25, 2024 hadi 02 Oktoba 2024,” imesema SRBG.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Ovin Ndimbo amesema ndugu walianza kujitokeza katika ofisi hizo kuanzia Agosti 2024 baada ya kupata taarifa zilizokuwa zinatolewa na mkandarasi huyo maeneo mbalimbali ikiwemo misikitini na makanisani.

“Zaidi ya watu 100 wamejitokeza waliozika ndugu zao karibu na barabara hiyo. Tunachokifanya kama viongozi kukusanya orodha ya watu wote halafu michakato mingine itasimamiwa na mkandarasi,” amesema Ndimbo.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo Kisiwani, Tatu Ally amesema waliozikwa katika eneo hilo ni wengi na kuna baadhi ya makaburi yamefutika.

“Eneo lilikuwa si rasmi la kuzika lakini lina makaburi mengi na watu walikuwa wanazika kiholela kwa kuwa tulikuwa hatutoi vibali hatukuwa na mamlaka nalo kwa sababu linamilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

“Hatuna idadi kamili ndiyo maana tunawaita watu wote waliozika ndugu zao waje kujiandikisha na kuonyesha walipowazika na baada ya hapo watakubaliana utaratibu utakuwaje? Kama kuwalipa fidia au kama kuna eneo lingine la kuzikwa limeandaliwa,” amesema Tatu.

Tatu amesema wao kama serikali za mtaa bado hawajui kama kuna eneo lingine limeandaliwa kwa ajili ya kuzika isipokuwa wakishapata idadi kamili watakubaliana kwa pamoja cha kufanya au kutafuta sehemu ya kwenda kuzika.

“Nafikiri wakishatambuliwa kwa kujulikana idadi kamili watakubaliana kwa pamoja na mkandarasi ni kiwango gani watapaswa kulipwa lakini kama uongozi wa mtaa bado hatujui,” amesema Tatu.

Tatu amesema waliozikwa katika eneo hilo wametoka maeneo mbalimbali ikiwemo Mabibo na Mazese na barabara hiyo inatakiwa kufukuliwa na kujengwa tatizo kuwapata ndugu wa marehemu imekuwa changamoto.

“Kuna makaburi mengi na baadhi yametitia na inawezekana wakianza kuchimba wataona mengine, hatuwezi kutoa bila ndugu kuwepo,” amesema Tatu.

Hamida Lissa miongoni mwa waliojitokeza kuandika jina lake baada ya ndugu yake kuzikwa katika eneo hilo tangu mwaka 2005 amesema kikubwa wanasubiria utaratibu.

“Nilifika hapa ofisini kuandika jina langu na namba yangu ya simu na kwenda kuonyesha karibu la ndugu yangu lilipo, nimeambiwa nirudi hadi watakaponipigisia simu ya kuitwa,” amesema.

Amesema kwakuwa serikali inataka kufanya jambo la maendeleo, kwake haina shida iwapo watakaa na kuzungumza pamoja na kukubaliana.

Related Posts