Ujenzi Daraja la Jangwani mbioni kuanza

Dar es Salaam. Serikali imesema Oktoba mwaka huu itasaini mkataba na mkandarasi atakayejenga Daraja la Jangwani.

Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ujenzi huo unatarajiwa kutumia miezi 24 hadi kukamilika baada ya mkataba kusainiwa.

Tanroads imeeleza hayo leo Septemba 26, 2024 katika mkutano na wahariri na waandishi wa vyombo jijini Dar es Salaam, ulioratibiwa na Msajili wa Hazina ukizungumzia mafanikio, changamoto na fursa za ofisi hiyo.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Ephatar Mlavi amesema ni ngumu kusema tarehe rasmi ambayo mkataba huo utasainiwa kwa sababu utahusisha viongozi wa ngazi za juu wanaotarajiwa kushuhudia.

“Hivyo lazima tushirikiane nao katika kupanga ratiba, kuendana na majukumu mengine wanayoendelea nayo, hatutaweza kusema tarehe kamili lakini ndani ya mwezi wa 10 (Oktoba) tuna matumaini makubwa kuwa mkataba huu utasainiwa,” amesema.

Mlavi amesema wakati mkataba huo ukisainiwa, ndipo kiasi cha fedha kinachotarajiwa kutumika hadi ujenzi utakapokamilika kitawekwa wazi.

Amesema taratibu zote za kisheria zitafuatwa hasa katika kuwaangalia wakazi wanaoishi karibu na eneo la ujenzi.

Mlavi ameeleza hayo ikiwa ni siku chache tangu, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alipolieleza Bunge kuwa taratibu za ununuzi zipo katika hatua za mwisho kabla ya kusaini mkataba huo.

Serikali imepanga kujenga daraja eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na kimo cha mita 15 ili kukabiliana na mafuriko.

Kwa mujibu Bashungwa, ujenzi wa daraja hilo utatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

Ujenzi huo utaenda sambamba na ulipaji fidia wananchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tamisemi kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Mkoa wa Dar es Salaam (DMDP II).

Katika hatua nyingine, Bashungwa alilielezea Bunge kuwa tayari Wizara ya Ujenzi imeanza kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa makandarasi waliokuwa wakisubiria fedha hizo ili waendelee na utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya barabara na madaraja.

Eneo la Jangwani mara kadhaa limekuwa likikumbwa na mafuriko kipindi cha mvua na kusababisha kufungwa kwa Barabara ya Morogoro, hivyo kuathiri shughuli za usafiri na usafirishaji.

Mlavi amesema Serikali imetumia Sh840 bilioni kufanya matengenezo ya barabara zilizoharibiwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.

Mbali na matengenezo hayo, amesema kilomita 15,343.88 zimekuwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji, huku kilomita 1,198.50 zikiwa zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema kilomita 2,031.11 ziko kwenye hatua za ujenzi kwa kiwango cha lami.

“Pia, kilometa 2,052.94 na madaraja mawili yamefanyiwa upembuzi yakinifu tayari kujengwa. Barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami,” amesema.

Mbali na hayo, amesema miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 5,326.90 na madaraja saba ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya kujengwa kwa kiwango cha lami.

Madaraja yanayotarajiwa kujengwa ni Godegode, Mtera – Dodoma, Ugala – Katavi, Kamshango, Kyabakoba na Kalebe – Kagera, Bujonde, Bulome, na Ipyana – Mbeya, Chakwale, Nguyami, Mkundi, Mjonga, Doma, Mkondoa – Morogoro, Lower Malagarasi – Kigoma, Sanga – Songwe, Kilambo – Mtwara  na Chemchem – Singida.

Amesema miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege inaendelea vikiwamo vya Msalato, Iringa, Musoma, Tabora, Shinyanga, Sumbawanga, Kigoma na Moshi.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts