Makonda: Vitongoji 186 vya Arusha kupelekewa umeme

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda amesema mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 186 wenye thamani ya zaidi ya Sh78 bilioni utawezesha kila mwananchi wa mkoa huo, kunufaika na huduma ya nishati hiyo.

Amesema kwa sasa vitongoji vyenye umeme ni 1,039 hadi lakini katika mradi ukitekelezwa utawezesha kufikia hadi 1,225 ambapo kwa lugha nyepesi watakuwa wakikaribia mpango wa kila kijiji cha mkoa huo kuwa na umeme.

Makonda ameeleza hayo leo Alhamisi Septemba 26, 2024 wilayani Arumeru wakati akimkabidhi zabuni mkandarasi atakayetekeleza jukumu la kusambaza umeme katika vitongoji 186 vinavyotokana na majimbo ya saba Mkoa wa Arusha.

Amesema Serikali imeamua  kupunguzia mzigo mwananchi na kwamba huduma ya  kuunganisha umeme itakuwa Sh27,000 kwa vijiji na vitongoji ili kila Mtanzania apate nishati hiyo ambayo ni kichagizo cha maendeleo kwa Taifa lolote linalotaka kuendelea.

“Kama upatikanaji wa umeme ni wa uhakika na gharama nafuu unawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kujikwamua kiuchumi,” amesema Makonda.

Katika hatua nyingine, Makonda amemtaka mkandarasi anayetekeleza jukumu hilo kulikamilisha kwa wakati, kwa sababu huduma ya umeme ni haki ya kila mwananchi wa Mkoa wa Arusha.

“Mkoa huu tuna utaratibu wetu hii pesa siyo mali ya serikali, hatutambeleza bali tunataka umeme na tunamtaka atumie vijana wa Mkoa wa Arusha katika kutekeleza majukumu yake kwa sababu hizi Sh78 bilioni ndiyo sehemu ya kuongeza uchumi wa vijana wetu

“Asitafute vijana kutoka sehemu nyingine, kwa sababu Arusha ina vijana kwa kila namna, utalaamu upo,tungemuomba atumie vijana wa mkoa huu ili mradi ukikamilika vijana hawa angalau wapaue nyumba zao,” amesema.

Mbali na hilo, Makonda amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan akisema hivi sasa changamoto ya mgao wa umeme imepungua tofauti na miaka iliyopota.

Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Mkoa wa Arusha una jumla ya vijiji 368 kati ya hivyo 362 sawa na asilimia 98.37 vimepata umeme. Pia kuna vitongoji ni 1,575 vitongoji vyenye umeme na huduma hiyo ni 545.

Related Posts