BILIONI 10 KUSAMBAZA UMEME KWENYA KAYA 2,700 KATIKA VITONGOJI 90 VYA MKOA WA SONGWE

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vitongoji (HAMLET ELECTRIFICATION PROJECT) kwenye vitongoji 90 vya majimbo sita (6) ya mkoa wa Songwe ambapo kaya 2,700 zitanufaika.

Akizungumza na Wanahabari ofisini kwake, leo tarehe 26 Septemba, 2024 wakati wa zoezi la kumtambulisha Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa huo katika mkoa wa Songwe, kampuni ya China Railway Construction Electrification Bureau Group Co. Ltd kutoka China; Mhe. Chongolo amesema kwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha Wananchi wa mkoa wa Songwe wanafikiwa na huduma ya umeme na kuongeza kuwa kila kijiji cha mkoa wa Songwe kimefikiwa na huduma ya umeme.

“Leo tunajivunia, vijiji vyote 307 vya mkoa wa Songwe vimefikiwa na nishati ya umeme, kazi hii siyo ndogo na tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa kufikisha huduma ya umeme kwenye mikoa ya pembezoni kama Songwe, kazi hiyo ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono na kupongezwa.” Amekaririwa Mhe. Chongolo.

“Tunampongeza sana, Mheshimiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameweka msukumo ili kuhakikisha Wananchi wanapata umeme na kuuona umeme siyo starehe bali ni huduma ya msingi ya kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao.” Amesema, Mhe. Chongolo.

Mhe. Chongolo ameipongeza REA kwa kuwasimamia Wakandarasi wanaosambaza huduma ya umeme kwa Watanzania na ametoa wito wa kuendelea, kuwasimamia Wakandarasi ili wakamilishe Miradi kwa wakati.

Viongozi wa REA; wakiongozwa na Mhandisi, Herini Mhina wamemwambia Mkuu wa mkoa wa Songwe kuwa kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 90 vya mkoa huo ilianza rasmi tarehe 20 Agosti, 2024 baada ya REA kwa niaba ya Serikali kusaini mikataba na Wakandarasi kwa lengo la kusambaza umeme kwenye vitongoji zaidi ya 3,000 kote nchi ambapo kupitia Mradi huo, mkoa wa Songwe umenufaika kwa kupata vitongji 90.

Katika taarifa yake ya awali, Mhandisi, Mhina amemwambia Mkuu wa mkoa wa Songwe kuwa Mradi huo, utahusisha ujenzi wa umeme wa msongo mdogo wa kilomita 180; kuunganisha Wateja wa njia moja 2,700 na kuunganisha Wateja wa njia tatu 270.

Alisema REA inatekeleza Miradi kwa kushirikiana na Viongozi wa maeneo husika na kwamba utambuzi wa vitongoji hivyo vya Mradi ulifanywa kwa kushirikisha Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo yote sita mkoani wa Songwe.

Naye Bwana Paranivel Kandasamil akiongea kwa niaba ya Mkandarasi alimuhakikishia Mkuu wa mkoa wa Songwe kuwa atatakeleza Mradi kwa mujibu wa mkataba na kwamba maandalizi yote muhimu yameshaanza na kwamba sehemu kubwa ya vifaa vimeshafika na kuahidi kumaliza Mradi huo katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.



Related Posts