Mchakato wa kumng’oa Naibu Rais wa Kenya waanza

Nairobi. Mpango wa kumwondoa Naibu Rais, Rigathi Gachagua kupitia kura ya kutokuwa na imani naye unazidi kushika kasi, huku baadhi ya wabunge wakisema wameambatisha saini zao kuunga mkono hoja hiyo.

Naibu Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kitaifa, Owen Baya alithibitisha jana jioni kuwa ukusanyaji wa saini za wabunge unaendelea na kwamba hoja hiyo itawasilishwa kwa wakati ufaao.

“Tumejenga kesi ya kuzuia maji. Hatutampa nafasi ya pili. Shughuli zake wikendi zilienda mbali sana,” Baya alisema.

Pamoja na kwamba alikataa kuzungumzia maelezo ya hoja hiyo ya kumfungulia mashitaka, alisema mara itakapofika vizuri bungeni, wabunge watatoa maoni yao.

“Hata walio pamoja naye wameelezea nia yao ya kutia saini hoja ya kumtimua wakisema kwamba atakapoondoka ofisini, mamlaka yake yataondolewa,” mbunge huyo wa Kilifi Kaskazini alisema.

Aliendelea: “Hii ni mbinu ya pande mbili na wanachama kutoka pande zote wakiunga mkono. Kila mtu anasema lazima amheshimu Rais. Hata wanaomuonea huruma wamemtelekeza, atabaki na wabunge wa zamani tu.”

Mbunge mwingine wa upinzani alisema mchakato huo unaendelea na huenda ukawasilishwa bungeni Jumanne ijayo.

“Litafanyiwa kazi wiki ijayo. Ukusanyaji wa saini unaendelea,” mbunge huyo alisema.

Wabunge kadhaa wamesema kuwa hoja hiyo itafikia bungeni kabla Rais William Ruto, ambaye kwa sasa yuko New York, Marekani kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA), kurejea.

Nation ya Kenya haijaweza kuthibitisha kwa uhuru nani atawasilisha hoja hiyo na ni wabunge wangapi hadi sasa wametia saini hoja hiyo.

Vyanzo vya habari viliiambia Nation kuwa mashtaka hayo yanahusu ukiukaji wa katiba na sheria nyinginezo, utovu wa nidhamu na matumizi mabaya wa ofisi, hasa kutokana na matamshi yake kwa umma waliyosema kuwa ni kutengwa na Wakenya wengine.

Kwa mujibu wa baadhi ya wabunge wanaofahamu matukio hayo, rasimu ya vipengee vya kumshtaki Gachagua vinagusia Ibara za 73, 75, 79, 129 na 131 za Katiba ya Kenya.

Baadhi ya “uhalifu” wa Naibu Rais ambao umewachefua wabunge ni pamoja na kauli yake mbaya katika Kaunti ya Kericho, Februari 2023 kuhusu umiliki wa hisa katika Serikali ya Kenya Kwanza, siasa za migawanyiko kwa kusema anausemea Mlima Kenya kwa gharama ya mikoa mingine, kukiuka Sheria ya Siri Rasmi na kutokuwa sehemu ya uwajibikaji wa pamoja wa baraza la Mbawaziri.

Pia, anashutumiwa kwa kushindwa kuheshimu ofisi yake kwa kujitenga hadharani na uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu Muswada wenye utata wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024. Wakati huo, alisema alikuwa akisikiliza msingi, na hivyo kukiuka uwajibikaji wa pamoja wa baraza la mawaziri na kudhoofisha imani ya umma kwa Baraza la Mawaziri.

Mahojiano yake ya hivi majuzi na kituo cha televisheni cha Citizen yanaelekea kutumiwa dhidi yake huku akishutumiwa kwa kujaribu kunyakua mamlaka ya Bunge kwa kusema kuwa kumshtaki kungesababisha ukosefu wa utulivu nchini.

Kutokana na hoja hiyo, sasa mwelekeo unaelekezwa kwa Spika wa Bunge na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Shughuli za Bunge kupanga ratiba ya jambo hilo.

Hadi kufikia jana usiku, wabunge wengi ambao Nation ilizungumza nao walikataa kuzungumza wakiomba uvumilivu ili kuwaruhusu kutekeleza majukumu yao kwenye ukumbi wa Bunge.

Pia, ilibainika kwamba washirika wa Rais Ruto walikuwa wameitisha mkutano katika hoteli moja Nairobi Jumanne usiku kujadili mkakati wa kumwondoa madarakani. Nation ilibaini kwamba angalau wabunge 30 walihudhuria mkutano huo ulioongozwa na Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Seneti, Aaron Cheruiyot.

Related Posts