Kampuni ya Mauritius yaishtaki Tanzania ikidai fidia Sh1.3 trilioni

Dar es Salaam. Kampuni ya Aqua Power Tanzania Limited imeishitaki Serikali ikidai fidia ya Dola milioni 500 za Marekani (zaidi ya Sh1.3 trilioni).

Kampuni ya Aqua Power yenye makao yake makuu, nchini Mauritius imefungua kesi katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), ikidai imebaguliwa kwa kunyimwa leseni ya uwekezaji katika sekta ya nishati, ikitaka kufidiwa zaidi ya Sh1.3 trilioni kwa kukosa biashara kwa miaka minne iliyopita na thamani ya miradi yao ya sasa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa nyaraka za shauri hilo ambazo Mwananchi imeziona, Aqua Power iliwasilisha maombi yake ya usuluhishi wa mgogoro kwa Katibu Mkuu wa ICSID kwa ajili ya usajili, Septemba 17, 2024 kupitia wakili Natasha Paray.

Mwanasheria, Govert Coppen kwa niaba ya Katibu Mkuu wa ICSID, iliijibu kampuni hiyo Septemba 18, 2024, ikithibitisha kupokea maombi hayo yaliyopewa namba ya usajili R20240074.

Septemba 18, 2024 ICSID kwa njia ya baruapepe iliwasilisha maombi hayo ya Aqua Power kwa Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari alipotafutwa hakupatikana kuzungumzia suala hilo, huku Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi akieleza waulizwe wenyewe.

Kwa mujibu wa hati ya maombi ya usuluhishi na notisi ya mgogoro huo, Aqua Power inadai mamlaka za Tanzania zimekiuka Mkataba wa Uwekezaji iliyoingia na Mauritius (BIT).

Inadai imebaguliwa kwa kunyimwa leseni, vibali na kutopewa malighafi ya gesi asilia kwa shughuli zake.

Kampuni hiyo inadai ilialikwa na Kampuni ya Dangote kuwekeza katika nishati kwa kujenga mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi na kuiuzia.

Kutokana na makubaliano hayo, ilijenga mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 45 mkoani Mtwara, ambao ulisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na iliwekeza Dola milioni 50 kwenye mradi huo.

Hata hivyo, inadai Serikali iliinyima leseni ya kuzalisha na kuuza umeme, badala yake ilielekeza leseni hiyo itolewe kwa Dangote, bila kujali Aqua Power ndiye mmiliki wa mtambo huo.

Inadai Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ilikataa kuiuzia malighafi (gesi asilia) kwa ajili shughuli zake, bila sababu halali.

Kampuni hiyo inadai Tanzania inasaidia upokonywaji wa rasilimali zake kwa ajili ya Kampuni ya CSI Energy Group (Tanzania) Limited, bila fidia yoyote kwake kama wamiliki na wawekezaji.

Kampuni hiyo inadai wakati ikinyimwa leseni na ridhaa ya kuzalisha umeme na kuiuzia Tanesco na nchi ya Msumbiji, ilitolewa awali kwa Kampuni ya Dangote na baadaye kwa Kampuni ya CSI kwa miradi ileile ya Aqua Power iliyosajiliwa na TIC.

Inadai matendo hayo yanasababisha uvunjivu wa ibara ya 3, 4 na 5 ya Mkataba wa Uwekezaji baina ya Mauritius na Tanzania (BIT).

Kabla ya kufungua shauri hilo, Septemba 26, 2023 kampuni hiyo ilitoa notisi ya miezi sita kwa Serikali ya Tanzania, ikieleza nia ya kuifungulia kesi, ikiialika kwa majadiliano, ili kufikia makubaliano kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya BIT kati ya Mauritius na Tanzania kuhusu kusuluhisha migogoro kati ya mwekezaji na nchi husika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi ya usuluhishi muda huo wa miezi sita uliisha Machi 31, 2024.

Inadaiwa kikao cha kwanza cha pande zote kilifanyika Machi 12, 2024 katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakakubaliana kukutana tena, lakini hakikufanyika, Tanzania ikiomba kwa mara kadhaa kiahirishwe na mara ya mwisho ilipangwa kifanyike Julai 9, 2024.

Hata hivyo, Juni 28, 2024, Serikali iliiandikia barua Aqua Power ikiifahamisha kuwa timu yake ya majadiliano isingeweza kukutana katika kikao cha pili kama kilivyokuwa kimepangwa kwa kuwa bado inasubiri ridhaa kutoka kwa mamlaka husika kuhusu suala hilo.

Inaelezwa hadi Septemba 17, 2024 Aqua Power ilipofungua shauri hilo kikao hicho hakijafanyika.

Katika notisi kampuni hiyo inadai imekuwa ikiwaandikia barua viongozi wa Serikali wenye dhamana, wakiwamo mawaziri kuhusu malalamiko hayo ili kutafuta ufumbuzi, lakini hakuna aliyejibu.

Related Posts