Samia akemea uzushi, akerwa viongozi kuwa bubu

Tunduru. Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kukerwa na tabia ya baadhi ya viongozi wanaoacha taarifa za uzushi zisambae bila kukanusha.

Amesema uzushi huo hutokea na kuyahusu maeneo yenye wawakilishi wa Serikali, lakini wanasubiri viongozi wa kitaifa wakanushe.

Kauli hiyo inatokana na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii taarifa zikionyesha picha ya mtu anayedaiwa kuwa mgonjwa aliyebebwa kwenye tenga kupelekwa hospitali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mgonjwa huyo mkazi wa Mchoteka wilayani Tunduru alibebwa kwenye tenga na kupakiwa kwenye pikipiki baada ya kushindwa kulipa gharama za kukodi gari la kubebea wagonjwa.

Rais Samia amesema hayo leo Septemba 26, 2024 alipozungumza na wananchi wa Tunduru, ikiwa ni siku ya nne ya ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma.

“Kama kunarushwa picha ya uongo katika mitandao, katika maeneo yetu kuna wakuu mbalimbali wapo, lakini hakuna anayekanusha, kwamba hiyo picha siyo ya leo.

“Kwamba hii hospitali au hilo eneo sasa hivi lipo katika hali hii na ikapigwa picha ikiwa katika hali hii kuondoa ule upotofu uliofanywa, sijui tunaelekea wapi,” amesema Rais Samia.

Amesema si sawa kusubiri Rais au waziri aende katika eneo husika akanushe uzushi, ilhali kuna viongozi ambao uzushi huo unawahusu moja kwa moja.

“Hii ni sawa mwanamume kaingia nyoka nyumbani kwako, unakwenda kumwita mwanamume mwenzio njoo nitolee nyoka nyumbani kwangu,” amesema.

“Kama kwenye nyumba yako unazushiwa, maendeleo yanakuja, fedha zinatoka, halafu anatokea mpuuzi mmoja anaweka picha za ajabu ajabu, lakini viongozi mmenyamaza kimya, mpaka Waziri aje awakanushie, mnatutia wasiwasi ndugu zangu,” amesema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameeleza kinachosambazwa ni uzushi.

Amesema kwa sasa hakuna changamoto ya ‘ambulensi’ kwa kuwa Serikali ilinunua magari hayo 530 yaliyosambazwa kwenye halmashauri.

Katika mgawo huo, amesema Halmashauri ya Tunduru imepokea magari manne kwa ajili ya kusambazwa kwenye vituo vya afya vya Nakapanya, Matemanga, Tunduru Kusini na Nalasi.

Amesema Tamisemi ina programu ya M-MAMA inayolipa fedha kwa madereva wa kijamii kuwabeba wagonjwa pale inapotokea gari la wagonjwa halipo.

Amesema kwa Tunduru Sh19 milioni zimetolewa kwa madereva 20 kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo.

“Picha hizi zinazosambaa zinalenga kuwachanganya Watanzania, kazi unayoifanya (Rais Samia) ni kubwa. Picha hizo za zamani,” amesema.

Mbali na hayo, Rais Samia ameeleza kuhusu uwepo wa soko la madini na ushindani unaowahakikisha wachimbaji na wauzaji bei na mapato zaidi.

Amesema hayo baada ya kuzindua soko la madini katika Wilaya ya Tunduru.

Amesema kati ya Julai na Agosti, 2024 Serikali ilipokea Sh6.3 bilioni kama maduhuli kutokana na madini mkoani Ruvuma.

“Ni mapato hayo ambayo yanatuwezesha kuja kufanya shughuli za maendeleo kama walivyosema wabunge wenu,” amesema.

Amesema eneo hilo kuna masoko mawili ya zamani, akimtaka Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kukaa na wachimbaji wadogo na sekta binafsi wazungumze kuona wanashirikianaje kufanikisha ujenzi.

Awali, Waziri Mavunde alisema katika siku 84 za mwanzo wa mwaka huu wa fedha, mauzo ya madini yameingiza Sh225 bilioni katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kiwango hicho cha fedha kilichoingizwa amesema ni matokeo ya uwepo wa masoko 43 ya madini na vituo 102 vya ununuzi wa rasilimali hiyo.

Akizungumzia mradi wa soko la madini Tunduru, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Chizya Marando amesema ujenzi umetekelezwa kwa ushirikiano na wafanyabiashara.

Ujenzi huo ulioanza Desemba mwaka jana, amesema umegharimu Sh1.4 bilioni na kati ya hizo, Sh1.37 bilioni zimetolewa na wafanyabiashara na Sh300 milioni ni halmashauri.

Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa ameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa madini ya urani ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Eneo la Mto Mkuju wilayani Namtumbo linaaminika kuwa na akiba kubwa zaidi ya urani nchini, ikiwa na tani milioni 182.1 za mabaki ya madini hayo.

Rais Samia amesema Serikali inashughulikia suala hilo.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts