Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, imesema pamoja na Serikali kuendelea kuongeza bajeti ya kilimo, bado haikidhi mahitaji halisi ya sekta hiyo kwa kuzingatia matakwa ya utekelezaji wa Azimio la Maputo (2003) na Malabo (2014) linalozitaka nchi wanachama kutenga asilimia 10 ya bajeti ya Taifa kwa ajili ya sekta ya kilimo.
Wizara ya Kilimo imeliomba Bunge kuidhinisha Sh1.248 trilioni zitakazotumika kwenye vipaumbele sita vyenye mikakati 27 katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Mwaka wa fedha wa 2023/24 iliomba kuidhinisha Sh970.8 bilioni, fedha zilizolenga utekelezaji wa vipaumbele vitano ambavyo ni kuongeza uzalishaji na tija, kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile amesema hayo bungeni alipowasilisha maoni ya kamati kuhusu bajeti ya Wizara ya Kilimo iliyosomwa leo Mei 2, 2024 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Amesema kamati inaishauri Serikali kuendelea kutenga bajeti na fedha zitolewe kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa malengo na mikakati iliyokusudiwa.
“Uzalishaji duni na usio na tija wa mazao ya kilimo unatokana na kukosekana mbolea ya kutosha na kwa wakati. Kamati inaishauri Serikali kuweka nguvu na kuchukua hatua za makusudi za kuzalisha pembejeo hapa nchini ikiwemo mbolea, mbegu na viuatilifu,” amesema.
“Pamoja na Serikali kuweka mfumo mzuri wa utoaji wa mbolea ya ruzuku nchini, bado mfumo huo haujafahamika ipasavyo kwa wakulima wengi, hivyo kutoleta tija iliyokusudiwa.”
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ameitaka Serikali kuweka bei elekezi ya zao la tangawizi ili kuinua uchumi wa wakulima nchini, wakiwamo wa jimbo hilo ambao wanazalisha asilimia 72 ya tangawizi yote inayozalishwa nchini.
Akichangia bajeti ya kilimo, amesema asilimia kubwa ya wananchi wa jimbo hilo ni wakulima wa zao hilo, hivyo wanahitaji miundombinu ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha biashara.
Amesema kati ya kilo 20,000 za tangawizi zinazozalishwa nchini, kilo 14,000 zinazalishwa Wilaya ya Same, hivyo ametaka bei elekezi ya zao hilo ili wakulima wanufaike kwani mpaka sasa hakuna bei iliyotolewa na Serikali.
“Sekta ya kilimo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 40 na hawa wakulima wa Same Mashariki wanaozalisha asilimia 72 ya tangawizi yote nchini wanahitaji kunufaika na kilimo chao, lakini changamoto kubwa hakuna bei elekezi ya zao hilo,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Jackline Msongozi ameitaka Serikali kuweka bei elekezi ya zao la mahindi inayofanana nchi nzima badala ya wengine kupewa bei kubwa na wengine ndogo wakati gharama wanazotumia kwenye kilimo zinafanana.
Amesema kuna baadhi ya mikoa hupewa bei elekezi ya Sh1,000 kwa kilo moja ya mahindi, huku wengine wakipewa Sh750 hali inayowakatisha tamaa wakulima.
Amesema hata kama bei hizo zitatofautiana ziwe ni kwa kiwango kidogo tofauti isifike Sh300.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ameitaka Serikali kuwasimamia wakulima wadogo kwa kupanua mashamba yao na kuwaunga kwenye ushirika ili waweze kuzalisha kwa tija.
Amesema wakulima wadogo ndiyo wanaolilisha Taifa kwa miaka yote, hivyo siyo busara kuwaweka kando na kushikamana na wakulima wakubwa tu, bali wawasaidie kuboresha mashamba yao ili waendelee kuzalisha kwa tija.
Ameitaka Serikali kutenga maeneo ya kilimo ili yasivamiwe na ujenzi wa makazi ili inapofika hatua ya kupanua mashamba kuwe na nafasi ya kutosha, badala ya kuweka uwekezaji mwingine kwenye mashamba.