STAA wa Simba, Debora Fernandes Mavambo amewaambia mashabiki bado ana vitu vingi ambavyo anaweza kuonyesha akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi kadri ambavyo atakuwa anazidi kuelewana na wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho.
Debora ambaye alizaliwa Februari 17, 2000, jijini Luanda, Angola, amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na namna ambavyo amenogesha eneo la kiungo cha timu hiyo.
Fundi huyo mwenye uraia wa Angola na Congo anakaba na kuchezesha jambo ambalo limekuwa likirahisisha mipango ya timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti staa huyo anayezungumza kireno, alisema licha ya kwamba anahisi mashabiki wameanza kumuelewa, anajiona bado kuna nafasi ya kuonyesha zaidi makucha yake kwa sababu anaendelea taratibu kuzoeana na wachezaji wenzake;
“Ndani ya muda mfupi ninajisikia furaha kuwa hapa, nilikuwa na wakati mzuri Misri ambako tuliweka kambi na kilikuwa kipindi kizuri kwangu kuanza kufahamiana na wachezaji wenzangu,”
“Nashukuru kocha alikuwa wazi kwangu na wachezaji wengine juu ya namna ambavyo anataka kuona timu ikicheza, tumekuwa tukifanya kazi kwangu kila mmoja ili kutoa kilichobora, binafsi najiona bado natakiwa kufanya zaidi ya hiki ambacho kwa sasa nakitoa, natakiwa kuonyesha thamani yangu zaidi.”
Debora anatambua ukubwa wa Simba na presha ambayo wachezaji wamekuwa wakikumbana nayo;
“Timu yetu ina wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa hivyo kila mmoja amekuwa akipambana kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara hilo nalo limekuwa likinisukuma pale ninapopangwa kwa kuthibitisha nastahili.”
Katika michezo minne ambayo Debora amecheza ya kimashindano, miwili Ligi Kuu Bara na mingine ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameonyesha ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi za kiungo wa kati na kiungo wa ulinzi.
Urefu wake wa mita 1.78 unampa faida ya kimwili uwanjani, akicheza kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu. Ameonekana kuleta utofauti kwenye eneo hilo huku akitumika sambamba na viungo wote kwa vipindi tofauti.
Katika michezo miwili ya kwanza katika ligi dhidi ya Tabora United na Fountain Gate, fundi huyo alikuwa akicheza na Mzamiru Yassin kama viungo wakabaji lakini kupata majeraha kwa mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, ilimbidi kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids kumtumia sambamba na Yusuph Kagoma katika michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripol.
Akiongelea kiwango cha mchezaji huyo, Fadlu alisema; “Debora ni mchezaji wa aina ya kipekee. Uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali za kiungo na nidhamu yake kimchezo ni sifa ambazo zinampa faida kubwa. Licha ya muda mfupi aliotumia nasi, ameweza kuendana na mfumo na kutoa mchango mkubwa.”