Madaktari bingwa wa Rais Samia, walioko katika kambi ya matibabu ya Hospitali ya Halmashauri ya Babati vijijini (Magugu), wamefanikiwa kumtoa kizazi mwanamke wa miaka 62 bila kufanyiwa upasuaji wa tumbo, katika operesheni iliyofanyika kwa njia ya ukeni. Mama huyo, mkazi wa kijiji cha Gichameda, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kushuka kizazi (uterine prolapse) kwa muda wa miezi sita.
Akizungumza Septemba 26, 2024, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya KCMC, Dkt. Chuma Novacatus, amesema kuwa mgonjwa huyo aliletwa hospitalini na mtoto wake baada ya kusikia taarifa za kambi ya madaktari bingwa ambapo awali alikuwa akipatwa na matatizo ya kutokwa na damu na maji maji ukeni, na awali amezunguka hospitali mbalimbali bila kupata matibabu sahihi.
“Mama huyu amezaa mara tisa, na alikuwa akisumbuliwa na kutokwa na damu. Tulipomfanyia vipimo, tuligundua kuwa kizazi kilikuwa kimeshuka na kutoka nje. Tumefanikiwa kukitoa kwa njia ya ukeni bila kupasua tumbo,” alisema Dkt. Novacatus.
Katika kambi hiyo, madaktari hao pia walimfanyia upasuaji mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 54 aliyekuwa na uvimbe kwenye kizazi, hali iliyosababisha maumivu na kutokwa na damu.Hata hivyo, wagonjwa wote wanaendelea vizuri na wako chini ya uangalizi wa madaktari.
“Wagonjwa wote hawa wanaendelea vizuri na wako wodini chini ya uangalizi wetu, nitoe wito kwa watanzania kufika hospitali na kutumia fursa ya wiki hii moja ya uwepo wa kambi ya matibabu ya madaktari bingwa wa Rais Samia ili kupatiwa huduma za kibingwa”. Dkt. Novacatus ametoa wito kwa wananchi kufika hospitalini ili kunufaika na huduma za kibingwa zinazotolewa katika kambi hiyo, ambayo itaendelea kwa muda wa wiki moja.