Aziz Ali, askari wa kikoloni aliyeacha jina la eneo Mtoni

Mtoni kwa Aziz Ali, ni eneo maarufu wilayani Temeke. Ni eneo lililo pembezoni mwa Barabara ya Kilwa likipakana na Viwanja vya Maonyesho ya Sabasaba na Mtongani.

Kwa mujibu wa mwanahistoria, Sheikh Mohamed Said, eneo hilo limebeba jina la Aziz Ali aliyefariki mwaka 1950, ikiwa ni miezi michache baada ya kutoka kuhiji katika Mji Mtukufu wa Makka uliopo Saudia Arabia.

Ni baba wa Dossa Aziz, mmoja wa wapigania uhuru maarufu na kiongozi wa TANU.

Inaelezwa  na nguli huyo wa historia kuwa Aziz alikuja Dar es Salaam mwanzoni mwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia akiwa askari wa Jeshi la Wajerumani na baadaye baada ya vita aliajiriwa na mfanyabiashara mmoja wa Kigoa.

Tajiri yake alimwachia magari mawili aliyotumia kufanya biashara na kisha kuanzisha kampuni yake ya ujenzi, akitajwa kama mtu mkarimu kwa watu aliokuwa akiwajengea nyumba.

‘’ Yeye alikuwa akitoa fursa kwa watu kumpa pesa kidogo kidogo kama malipo ya nyumba alizokuwa anawajengea na alikuwa mtu akishindwa kulipa akimpa muda hadi atakapoweza,’’ anamwelezea katika andiko lake alilochapisha katika mtandao wa Jamiiforums mwaka 2018.

Kwa mujibu wa Sheikh Mohamed Said, jina lake halisi ni Ali Kidonyo mwenyeji wa Tanga, aliyepewa jina Aziz yaani kipenzi na watu.

Umaarufu na wema wake ukatosha kuacha alama kwa eneo alilokuwa akiishi kupewa jina lake. Hii ndiyo asili ya Mtoni kwa Aziz Ali.

Akimsimulia Aziz Ali katika moja ya machapisho yake, Said anaandika:

‘‘Kwa hakika jina lake hasa ni Ali Kidonyo.Hili ndilo jina lake alilojulikana akiwa mtoto na kisha akiwa kijana huko kwao Tanga.

Hili jina la Aziz alipewa na watu wa Dar es Salaam kwa hisani na wema wake.

Yeye alikuwa akitoa fursa kwa watu kumpa pesa kidogo kidogo kama malipo ya nyumba alizokuwa anawajengea na alikuwa mtu akishindwa kulipa, basi anampa   muda hadi atakapoweza.’’

Anaendelea: ‘‘Nyumbani kwake mwezi Mtukufu wa Ramadhani  ulipokuwa ukifika, alikuwa akitandika nje majamvi na kufuturisha hadi watu 100 asiowajua wakija wanafuturu na kuondoka.

Ndipo wakamwita “Aziz” yaani “Mpenzi.” Ikawa wakimtaja jina wanatanguliza “Aziz,” yaani “Kipenzi chetu Ali.”

Jina la awali la eneo hilo

Zipo simulizi zinazoeleza kuwa kabla ya kuitwa ka Azi Ali, eneo hilo liliitwa Magogoni na kuliwahi kuwapo kwa makazi ya wapiganaji wa chama cha Frelimo kutoka Msumbiji.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts