NILIKUWA natazama mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Pamba na Mashujaa FC iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba wiki iliyopita.
Kosa la kipa Yona Amos lilichangia kuinyima timu ya Pamba ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kushindwa kuokoa shuti la mbali la David Ulomi Richard.
Ndio lilikuwa ni kosa la Yona. Hakuna namna unaweza kumtetea kwa lile bao maana alikuwa amesimama mahali sahihi langoni na mpira ukapita hapohapo lakini akashindwa kuzuia shuti hilo ambalo liliipa Mashujaa sare muhimu ugenini.
Kwa mtazamo chanya lile ni bao ambalo Yona Amos alipaswa afungwe kwa faida yake mwenyewe na hata Pamba baada ya kupita kipindi kirefu cha kupokea sifa kutoka kwa wadau wengi wa soka nchini kuwa ni miongoni mwa makipa bora nchini.
Inawezekana sifa zingeendelea kumfanya awe anajisahau na kubweteka na hivyo ingeweza kumfanya mbele ya safari aporomoke kiwango na hivyo kumsababishia ashindwe kufikia malengo.
Kosa kama lile litamjenga na kumuongezea umakini zaidi ambao utakuwa na faida kwake na timu anayoichezea na hivyo ataendelea kujituma zaidi ili awe na ubora wa hali ya juu.
Tukumbuke kuwa Yona ni miongoni mwa makipa ambao wamekuwa wakiitwa katika kikosi cha timu yetu ya taifa, Taifa Stars na inawezekana siku moja akapewa jukumu la kulinda milingoti mitatu ya lango la timu hiyo katika mashindano makubwa.
Hapo atacheza dhidi ya wachezaji wa daraja la juu ambao kosa moja tu la kujisahau kwa kipa pindi awapo golini wanaweza kulitumia vyema kuiadhibu timu na mwisho wa yote kuifanya Taifa Stars ishindwe kutimiza malengo.
Lakini kosa kama la juzi linapotokea kwa ngazi ya klabu tena katika mechi za mwanzo za ligi, Yona Amos atacheza kwa tahadhari kubwa mechi zake na umakini wake utakuwa wa hali ya juu kwa dakika 90 ili kuepuka kurudia hilo jambo ambalo litakuwa na manufaa kwake.