“Dkt.Tulia amerejesha furaha” Mbunge Fyandomo akoshwa na ushindani,burudani ya Ngoma za asili

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya Suma Fyandomo, amesema mashindano ya ngoma asili yanayoendelea jijini Mbeya yameibua ari na nguvu kwa vikundi na wasanii kuendelea kutoa burudani kupitia ngoma asili ambazo zilionekana zikiendelea kufifia kutokana na nguvu ya muziki wa kizazi kipya (Bongo flava).

Ameeleza hayo wakati akiongea Ayo TV pamoja na Millardayo.com jijini humo wakati shindano la ngoma asili likiendelea ambapo amesema kitendo cha Dkt.Tulia Ackson Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania kuipa nguvu ngoma asili kumeendelea kudumisha utamaduni wa ngoma.

“Kwa namna anavyoandaa mashindano ya ngoma anadumisha utamaduni ambao ni asili yetu unajua kwa kipindi kirefu sana ngoma hizi ni kama zilififia lakini sasa hivi amerejesha furaha tena kwasababu zile ngoma zote zilizopo kwenye wilaya zetu zinaibuka na hawaishii hapa tu, wakirudi kwao wanaendelea kudumisha ngoma ambao ndio utamaduni wetu”amesema mbunge Fyandomo

Awali mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera akizindua jukwaa hilo la utamaduni “TULIA TRADITIONAL DANCE FESTIVAL 2024” yanayofanyika uwanja wa ndege wa zamani ikiwa ni msimu wake wa nane amesema wanambeya wanakila sababu ya kuendelea kuiunga mkono serikali pamoja na mbunge wao kutokana na jitihada kubwa za maendeleo wanazofanya kwenye mkoa huo huku pia akitoa wito wananchi kujitokeza kwenye chaguzi zinazokaribia.

“Ndugu zangu wabunge wetu wanaendelea kufanya kazi kubwa ndio maana hospitali ya kanda tumeendelea nayo,tunajenga barabara ya njia nne na Mh Rais amemlipa mkandarasi Bil.tisa kwa heshima ya Dkt.Tulia na wana mbeya,soko matola tumevunja pale tunajenga soko la kisasa na stendi mpya ya kisasa hapa”amesema Homera

Tamasha hilo la ngoma asilia lililoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust linahusisha vikundi zaidi ya 150 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania limepelekea kuwa na ushindani mkubwa kutokana na umahiri wa vikundi vilivyojitokeza ambapo baadhi ya washiriki ikiwemo ngoma ya Mganda kutoka mkoani Njombe wamemshukuru mbunge wa Mbeya mjini Dkt.Tulia kwa kuwatengenezea fursa ya ushindani.

Related Posts