Iringa. Watoto watatu, mmoja kati yao akiwa wa kiume, wamebakwa na kulawitiwa na mtu ambaye aliwakamata akijifanya ni askari polisi katika Mtaa wa Dodoma Road E, Kata ya Mkimbizi iliyopo katika manispaa ya Iringa.
Watoto hao wenye umri wa miaka kati ya 13 – 15 (majina yanahifadhiwa), wamefanyiwa ukatili huo April 30, 2024 baada ya mtu huyo aliyejifanya kuwa ni askari polisi kuwakamata akidai anawapeleka ofisi za kata kwa kosa la kutembea usiku.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanamtafuta mtu huyo ambaye alijifanya askari.
Wakizungumza na Mwananchi nyumbani kwao leo Mei 2, 2024, Mtaa wa Dodoma Road E, watoto hao walidai awali walitumwa dukani na wazazi wao lakini walipofika eneo la Mwembeni walimkuta mtu, ambaye aliwauliza wanakokwenda.
“Sisi tulisema tunaenda dukani, ndio akasema anatukamata kwa sababu tunatembea usiku, akasema tumfuate, tukaanza kumfuata mbele tukamkuta mvulana ambaye pia alitumwa dukani, akasema nae aongozane na sisi,” amesimulia mtoto mmoja.
Mtoto mwingine amesema waliongozana na mtu huyo, wakafika kwenye nyumba ambayo watu wakipita inawaka taa na ndani mbwa wanapiga kelele.
“Akasema tusipite njia hiyo kwa sababu taa zitawaka na mbwa watapiga kelele, tukipita hapo watakuwa askari wengine watatukamata yeye anatuhurumia. Basi akazunguka na sisi nyuma, tukaenda hadi kule mlimani ndio akatufanyia hivi. Tulijaribu kupiga kelele lakini hatukuweza,” amesimulia mtoto mwingine.
Mmoja wa wazazi wa watoto hao amesema baada ya kuwatuma watoto hao dukani, alishangaa kuona muda mrefu unapita lakini hawarudi.
“Ikabidi twende kwa mwenyekiti wa mtaa kutoa taarifa juu ya watoto kutoonekana, tulihisi wametekwa,” amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Dodoma Road E, Abeid Kamtande amesema siku ya tukio wanawake wawili walifika nyumbani kwake na kueleza kuwa wametekwa.
“Walikuja wanalia, nikashangaa wanalia nini, wakasema watoto walitumwa dukani majira ya saa moja usiku, lakini wametekwa na hawajarudi nyumbani. Kweli ilibidi nitoke, tukawafuata wajumbe na watu wa ulinzi shirikishi, tukampigia polisi kata na kuanza kuwatafuta,” amesema.
Amesema waliwagawa watu hao kwenye makundi matatu kwa lengo la kuwatafuta huku wengine wakipita njia ambayo watoto hao walipita.
“Tulizunguka hadi Mkimbizi kuwatafuta watoto lakini hatukufanikiwa, nikawauliza wazazi, si tumepiga marufuku watoto chini ya umri wa miaka 18 kutembea usiku? Wakakiri kuwa kweli hilo walikosea. Basi tulihangaika mpaka baadae ndio tukawaona watoto,” amesema.
Takwimu zinaonyesha kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili wa kingono kwa watoto yamekuwa wakishika kasi licha ya jitihada mbalimbali.