Dar es Salaam. Katika kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuimarisha afya ya uzazi kwa vijana balehe kati ya miaka 10 mpaka 19 walio ndani na nje ya mfumo wa shule, Taasisi ya Apotheker imeanzisha mradi wa Afya-Tek utakaowakusanya kupitia vilabu na kampeni kidijitali.
Miongoni mwa changamoto zinazolikabili kundi hilo ni pamoja na tabia hatarishi ikiwemo kujiingiza katika makundi yasiyofaa, uvutaji wa sigara, shisha na pombe za mtaani.
Afya-Tek inalenga kuboresha ustawi wa watoto, vijana na familia zao, kupitia matunzo yanayowezeshwa kidijitali, ambapo kwa sasa wameanza na mkoa wa Pwani.
Akizungumza katika mahojiano maalum jana Septemba 26, 2024 na Mwananchi, Daktari bingwa wa afya ya watoto, Suleiman Kamatta amesema katika umri huo kila mtoto anataka kujaribu kila kitu.
“Wanapata majaribu makubwa na ndiyo wakati ambao wanapata wenzao wa rika wasio na maadili mazuri wanawafuata kirahisi. Hiki ndiyo kipindi ambacho watoto wanaanza kuvuta bangi, sigara, kunywa pombe na wana vinywaji vingi wanavinywa kama ‘double kiki’, visungura na bia za kawaida wanavuta mpaka shisha,” amesema.
Dk Kamatta amesema vitu hivyo huwafanya hata akili zao zisiwe za kawaida, wanaingia humo na kuwa hawajeuri hawasikii malezi mazuri, wanatofautiana na wazazi wao hivyo nguvu nyingi inabidi iwekwe wawe na maadili mema na wajifunze vizuri.
Dk Kamatta ambaye pia ni mtaalamu anayeshughulika na sera katika shirila la Apotheker, amesema vijana kati ya miaka 10 mpaka 19 wanapata matatizo makubwa hasa ya mimba za utotoni huku asilimia kubwa wakiwa bado katika masomo.
“Wasichana wa umri huo kuanzia shule za msingi na sekondari shule ya msingi, wanapata mimba na huu umri ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa vifo vitokanavyo na uzazi,” amesema.
Amefafanua kuwa bado kuna changamoto ya kuwafikia vijana hao hasa walio nje ya mfumo wa shule.
“Tuliona njia bora ni kuanzisha klabu kwa vijana walio shuleni na huko ni rahisi kuwapata wanaendeshewa mada nyingi na mojawapo ni afya ya uzazi.
“Walio nje ya shule nao wanaanzishiwa klabu lakini uanzishwaji wake lazima kuanza na muundo wa serikali za mitaa au vijiji, sasa pale wao wenyewe ndiyo watakuwa walezi wa hizo klabu. Tumeshaanzisha klabu kama hizo 41 katika halmashauri ya Kibaha.”
Dk Kamatta amesema katika klabu hizo wanatoa mafunzo mbalimbali ikiwemo mijadala ya mimba za utotoni, vijana wanajadiliana kwa undani ingawaje si rahisi kuwapata.
“Hizi mada zinazungumzika, sasa tuna wataalamu wa vituo vya huduma za afya, wataalamu wa halmashauri, hospitali za wilaya na halmashauri kwenye hayo maeneo kuhusu mimba za utotoni kwani ni kipindi muhimu kwao kupata mwongozo barabara,” amesema
Hata hivyo, amesema kuna tofauti katika kuelezana na vijana wa kiume na hali ya afya kwa vijana wa kike kwakuwa mijadala yenyewe inatakiwa iendeshwe kwa umakini mkubwa ili kufikisha ujumbe barabara.
Dk Kamatta amesema lazima njia za kulifikia kundi hili zipanuke kwa watoa ili watoa mada waweze kuwadikia na kushauriana na vijana ikiwemo kufika shuleni na kutoa elimu hasa katika vipindi maalum.
“Walio nje ya shule zifanyie jitihada nao waweze kufikiwa na wataalamu wawapatie elimu kwakuwa hawafiki kwenye vituo vya kutolea huduma za afya hawafiki sasa tuwatafute na vituo vyetu vya huduma za afya lazima viwe rafiki kwa huu umri,” amesema.
Pia amewaasa wazazi na walezi wasiwe wagumu na kwamba wasikae na kufikiria kwamba haya mambo wao hawahusiki sana kuwaeleza watoto wao, bali wawe wawazi mama akae na binti amweleze masuala ya afya ya uzazi, baba naye asikae mbali na hawa watoto awaeleze na jamii iache miiko.
Dk Kamatta amesema kama sehemu ya mradi huo, wanatarajia kuwa na mdahalo Zanzibar Oktoba mwaka huu ambao wabobezi watakaa kuongea mada itakayohusu mradi wa Afya-Tek hasa wakiongelea jinsi wanavyotumia mfumo uhusiano PPP umma na binafsi katika kuboresha afya ya jamii na matumizi ya teknolojia.