KIPA wa Simba, Moussa Camara amezungumzia ubora wa ukuta wa timu hiyo unaongozwa na Fondoh Che Malone na Abdulrazack Mohamed Hamza kama sehemu ya kufanya kwake vizuri katika michezo mitano iliyopita katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ameruhusu bao moja tu.
Camara aliyecheza kwa umahiri mkubwa jana usiku katika mchezo wa ligi dhidi ya Azam uliopigwa visiwani Zanzibar na Simba kushinda mabao 2-0, huku akichaguliwa Nyota wa Mchezo, alisema hakuna maajabu kwake zaidi ya ushirikiano mzuri ambao amekuwa akiupata kwa wachezaji wenzake.
Kipa huyo aliyasema katika mahojiano maalumu na mtandao wa Simba na kusema;
“Najisikia vizuri sana. Tumefanya kazi kubwa kwa sababu ilikuwa mechi muhimu na tumefanya kila juhudi kushinda. Nafurahi sana kwa jinsi tulivyofanikisha ushindi huu katika mchezo huu mkubwa.”
“Tumekuwa tukifanya kazi kwa ushirikiano, Malone na Hamza wamekuwa na mchango mkubwa na hata Chamou Karaboue, Kapombe, Tshabalala na timu kwa jumla bila wao ni ngumu kucheza bila ya kuruhusu bao, naamini tutaendelea kuwa bora zaidi.”
Camara alisisitiza mechi dhidi ya Azam ilikuwa muhimu kwa Simba kuibuka na ushindi ili kuendelea na harakati zao za kujaribu kupambania ubingwa wa ligi.
“Tulicheza vizuri, ni furaha kuwa sehemu ya ushindi huu. Lengo letu ni kushinda michezo mingi na kuchukua ubingwa mwishoni mwa msimu,” aliongeza kipa huyo wa kimataifa kutoka Guinea.
Kuhusu clean sheet tatu alizonazo hadi sasa ndani ya michezo hiyo, Camara alisema ni heshima kubwa kwake kuwa sehemu ya timu kubwa kama Simba.
“Ninajivunia sana kuwa hapa na kusaidia timu yangu. Nawashukuru benchi la ufundi, hasa kocha wa makipa, kwa kuniongoza na kunisaidia kufika hapa. Simba ni klabu kubwa na ni furaha kwangu kuwa sehemu yake,” alisema kwa furaha.
Camara pia alizungumzia mechi inayofuata dhidi ya Dodoma Jiji FC, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushinda.
“Tunahitaji kujikita kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Dodoma. Tunajua itakuwa mechi ngumu, lakini tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kuchukua pointi muhimu,” alisema Camara.