Arusha. Kitendawili cha kupatikana kwa mwanafunzi, Joel Johannes aliyepotea akiwa na wanafunzi wenzake waliopanda Mlima Kwaraa mkoani Manyara kwa ajili ya ziara ya mafunzo, bado ni kigumu.
Joel mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara mwenye umri wa miaka 14, alitoweka tangu Septemba 14, 2024 katika mlima huo ulipo wilayani Babati mkoa wa Manyara, ambapo yeye na wanafunzi wenzake 102 walipanda mlima siku hiyo wakiwa na walimu wao na waongozaji.
Licha ya juhudi za kumtafuta mwanafunzi huyo ikiwemo kwa kutumia ndege isiyo na rubani katika mlima huo, mgambo 60 walioungana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wananchi kumsaka mwanafunzi huyo, bado juhudi hizo hazijazaa matunda.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Septemba 27, 2024, Katibu Tawala Wilaya ya Babati, Halfan Matupula, amesema wanaendelea kumtafuta mwanafunzi huyo.
“Mwanafunzi anaendelea kutafutwa, bado hajapatikana,” amesema Halfan kupitia ujumbe mfupi wa maandishi.
Akizungumza kwa njia ya simu, baba wa mtoto huyo, Johannes Mariki amesema bado hawajakata tamaa na kuwa licha ya Serikali kuendelea kumtafuta na wao bado wanazunguka mitaani kumtafuta kijana wao.
“Uongozi wa Serikali umesema unafuatilia na sisi tumewaachia na leo ni wiki ya pili hatujui alipo.
“Hatuwezi kuingilia Serikali ila bado hatujarudi kwetu Arusha tutaendaje mtoto hajapatikana? Bado hatujakata tamaa ndiyo maana tuko huku hadi leo mimi na familia yangu,” amesema
Septemba 23, 2024, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, alisema uchunguzi wa awali umebaini Joel hakufika kwenye kilele cha mlima pamoja na wenzake kama ilivyotarajiwa na kuwa jeshi hilo linaendelea kumtafuta huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini kilichotokea.
“Hatujampata mwanafunzi bado kilichoonekana katika uchunguzi wa awali hakupanda juu ya mlima, licha ya kumtafuta hadi tumetumia droni lakini hatukumpata.
“Baada ya kuchakata taarifa za mwanzo ikiwemo kwa wenzake, ni wazi hakupanda mlima licha ya kumtafuta kwa siku kadhaa, tunaendelea kumtafuta nje ya mlima ule ili tujue alipo,” ameongeza Kamanda huyo
Awali mkuu wa shule hiyo, Emanuel Dahaye, alisema katika mazingira ya sasa wanahisi mwanafunzi huyo ametoroka na yuko mtaani, hivyo nguvu ya kumtafuta kuelekezwa mtaani nje ya mlima huo.