Dar es Salaam. Kama una tabia ya kuchelewa kula usiku, basi unakabiliwa na hatari ya kupata magonjwa ya moyo, hususani wale wanaotumia vyakula vyenye wanga na sukari.
Takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 17 wanakufa kwa magonjwa ya moyo duniani kwa mwaka na tatizo hilo linaongezeka kwa nchi zinazoendelea, ambapo kwa Tanzania ya vifo vikifikia asilimia 13, huku gharama za matibabu zikiwa kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 27, 2025 kuhusu maadhimisho ya Siku ya Moyo duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema ulaji sahihi wa vyakula unaweza kumwepusha mtu na magonjwa ya moyo.
“Kutozingatia lishe bora kama vile kutumia sukari nyingi, wanga unatumia wakati umechelewa kula ambapo unakula katika muda umezidi, mfano unapokula usiku sana unachangia unene ambao ni rahisi kupata magonjwa haya ya moyo,” amesema Dk Kisenge.
Pia, Dk Kisenge amesisitiza kuepuka lishe duni na kufanya mazoezi ya mara kwa mara, ili kuboresha afya ya moyo, huku akishauri kutokunywa pombe kupita kiasi na kuacha kuvuta sigara.
Kuhusu maadhimisho hayo, amesema JKCI) wameandaa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo Septemba 29, 2024 kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani.
Amesema kambi hiyo itakuwa katika tawi lao jipya lililopo Kawe na kutakuwa na madaktari bingwa wa moyo pamoja na wataalamu wa lishe watakaotoa elimu.
“Wataalamu wa lishe watatoa elimu ya lishe bora itakayowapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza, yanayoweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu,” amesema Dk Kisenge.
Zuhura Hussein, mkazi wa Kinondoni amesema amekuwa na kliniki ya moyo akiamini ni uzembe wake mwenye ambao kwa sasa unamgharimu pesa nyingi kwa ajili ya matibabu.
“Kupata maradhi haya sikutarajia niliamini wanaopata ni watu wazima nikawa nakula na kulala kwa sababu sifanyi shughuli yoyote nipo nyumbani na kunenepa niliona ji kawaida kumbe nilikuwa nakaribisha maradhi,” amesema Zuhura.
Amesema umri wake na mwili haviendani kwani anaonekana mtu mzima wakati ana miaka 24 na sasa anaonekana kama mwenye miaka 40 na amegundulika ana moyo mkubwa.