Ni kama historia inakwenda kujirudia kwenye siasa za Kenya. Ilianza kwa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto kiasi cha kuharibu mambo kuanzia ofisini, kwenye kampeni na hata baada ya uchaguzi uliomuweka Dk Ruto madarakani.
Kwa sasa ni zamu ya Ruto tena na Naibu Rais wake, Rigathi Gachagua. Hawapikiki chungu kimoja na uadui umeanza kuchukua nafasi.
Gachagua amekalia kuti kavu na muda wowote anaweza kuondolewa kwenye wadhifa huo kupitia hoja itakayowasilishwa bungeni na washirika wa Ruto.
Kwa upande mmoja wa malumbano hayo ni Rais na viongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) wanaoumuunga mkono na upande wa pili ni wa naibu wake na viongozi ambao wamesimama naye.
Hatua ya hivi karibuni inayoashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya wawili hao ni ile ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki kutangaza kuwa Serikali itawafungulia kesi baadhi ya viongozi wanaodaiwa kupanga na kufadhili maandamano ya vijana.
Maandamano hayo yaliitikisa Serikali katika ya mwezi Juni na Julai, mwaka huu. Wanaohusishwa na njama hizo ni washirika wa Gachagua.
Kama haitoshi, juzi Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilipendekeza washirika wa karibu wa Gachagua washtakiwe kwa kupanga maandamano ya vijana yaliyotikisa nchi.
Katika barua hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, amependekeza mashtaka dhidi ya wabunge Benjamin Gathiru Mwangi (Embakasi ya Kati) na James Mwangi Gakuya (Embakasi Kaskazini). Wengine ni George Theuri, Martin Deric na Ngunjiri Wambugu ambao, Gachagua alisema ni wafanyakazi wa ofisi yake.
“Hili ni jaribio la kuchafua jina langu na kutoa sababu za kuniondoa mamlakani,” alisema Gachagua alipozungumzia tuhuma hizo.
Ni mzozo kama huo ndio ulivuruga uhusiano kati ya Uhuru na Ruto, ambao hawakuwahi kukubaliana kwenye suala la maridhiano na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.
Mpaka Uhuru anaondoka madarakani mwaka 2022, uhusiano wake na Ruto haujatengamaa mpaka sasa na kwenye uchaguzi alimuunga mkono Raila. Katika kulipiza, Ruto alianza kuminya mianya ya Uhuru na kusumbua familia yake.
Kwa sasa Ruto anafuata njia ya Uhuru kwa kufanya mazungumzo na Raila ikiwemo kumuunga mkono kiongozi huyo wa ODM katika kinyang’anyiro cha kuwania Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
Katika mahojiano aliyofanya na televisheni ya Citizen Ijumaa Septemba 20, 2024, Gachagua alifunguka akitaja chanzo cha mzozo kati ya Ruto.
Alisema Ruto ndiye aliyemfuata na kumuomba awe mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa sababu alisimama naye kidete alipokuwa akisumbuliwa na Serikali ya Jubilee.
Alisema, Ruto aliahidi familia yake; mkewe, Pasta Dorcas Gachagua na wanawe, kwamba hatampitishia madhila aliyopitia endapo angeibuka kidedea, katika kinyang’anyiro dhidi ya Raila.
Alieleza kushangazwa na ukimya wa Rais Ruto wakati uhusiano wao ukiyumba, huku baadhi ya viongozi wakimrushia vijembe.
“Ukweli ni kwamba ninadunishwa na baadhi ya viongozi serikalini, ninahitaji heshima kama Naibu Rais wa Kenya,” alisema Gachagua.
Alisema baada ya ‘Handisheki’ kati ya Ruto na Raila, kauli aliyopewa na Rais kuhusu ujio wa Raila serikalini, imegeuka kuwa jukwaa la kutaka kumuondoa mamlakani.
Miongoni mwa kejeli alizozitaja ni kutoka kwa ofisa mmoja mkuu serikalini aliyemtukana katika uwanja wa ndege ambao hakuufichua.
“Majuzi, ofisa mmoja mkuu serikalini alinitukana mara tano katika uwanja wa ndege,” Gachagua alisema.
Gachagua alilalamikia hadhi yake kudunishwa ndani ya Serikali aliyoshiriki kuiunda mwaka 2022.
Septemba 15, 2024, kiongozi huyo hakuwepo kwenye ziara ya Ruto katika eneo la Nyeri linalotajwa kuwa ngome ya Gachagua. Badala yake, alihudhuria ibada ya Kanisa Kaunti ya Kirinyaga.
Kiongozi wabunge walio wengi Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah, aliyeandamana na Ruto katika ziara hiyo, alimtaka kiongozi wa nchi kuwaondoa serikalini baadhi ya viongozi wakuu aliodai wanakwamisha jitihada zake za kuhudumia wananchi.
Ichung’wah alitumia jina ‘nyoka’, akiashiria viongozi hao japo hakuwataja kwa majina yao.
Gachagua amelaani matumizi mabaya ya mfumo wa haki kuwasumbua washirika wake kwa sababu ya misimamo ya kisiasa, huku akionekana kumnyooshea kidole Ruto,
Amemkumbusha Ruto kwamba, aliahidi Wakenya kuwa chini ya utawala wake, maofisa wa usalama hawatatumiwa kudhulumu watu kisiasa.
“Rais William Ruto na mimi, tulipoingia mamlakani tulitoa ahadi kwa watu wa Kenya kwamba, kamwe mfumo wa haki hautatumiwa tena kushughulikia tofauti za kisiasa.
“Naona aibu tumerudi pale tulipokuwa. Unyanyasaji wa watumishi wa ofisi yangu na wabunge wanaoonekana kuwa karibu na mimi umekuwa ukiendelea kwa muda wa miezi miwili iliyopita,” alisema.
Wakati huohuo, joto la kisiasa likizidi kupanda, mipango ya kuwasilisha hoja bunegni ya kumtimua inaelezwa kuwa imekamilika.
Zaidi ya wabunge 116 tayari wameripotiwa kuidhinisha hoja ya kumtimua kwa madai ya ukiukaji wa mara kadhaa wa Katiba ya Kenya.
Imeelezwa kuwa mashtaka hayo yanahusu ukiukaji wa Katiba na sheria zinazohusiana, utovu wa nidhamu uliokithiri na matumizi mabaya ya ofisi, hasa yakijikita kwenye kauli zake kama vile ‘serikali ya hisa’, ambayo ni sawa na kuwatenga Wakenya wengine.
Baadhi ya makosa ambayo Gachagua anatajwa kuyafanya ni pamoja na kauli yake maarufu katika Kaunti ya Kericho, iliyoitoa Februari mwaka jana kuhusu umiliki wa hisa katika Serikali ya Kenya Kwanza.
Pia, kuna madai ya siasa za migawanyiko, akidaiwa kupendelea zaidi eneo la Mlima na kubagua mengine na ukiukaji wa usiri serikalini kuhusu shughuli za Baraza la Mawaziri.
Washirika wa Ruto walikasirishwa na kauli ya Gachagua dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji, katika kilele cha maandamano ya Gen Z ambayo yalishuhudia uvamizi bungeni. Wanadai kuwa kauli yake ilihatarisha usalama wa Kenya.
Pia, anashutumiwa kwa kutoheshimu ofisi yake kwa kujitenga hadharani na uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu Muswada tata wa Fedha wa 2024, ambao uliondolewa.
Haya yanajiri huku ikidaiwa kuwepo kwa washirika wa Ruto kufanya mkutano wa siri kwenye hoteli moja ya Nairobi, kujadili mkakati wa kumtimua Gachagua.
Katika mkutano huo ilielezwa kuwa karibu wabunge 30 walihudhuria na ulioongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, na suala la kumuondoa Gachagua lilijadiliwa.
“Ilikubaliwa kuwa ukusanyaji wa saini uanze, lakini kuwasilishwa kwa hoja kutapangiwa tarehe maalumu,” chanzo kililiambia gazeti la Taifa Leo.
Mbunge wa Kimilili, Didmus Baraza alithibitisha kuwa atatia saini kuunga mkono hoja hiyo.
Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa, Gladys Shollei ni miongoni mwa wanaotaka Gachagua atimuliwe.
“Ninakuonya Gachagua, utaondolewa madarakani na ninaweza kukuthibitishia hili na nitasimamia hoja ya kukutimua,” alisema Sholei.
Baada ya kuona vita vimekolea, Gachagua ameonekana akituliza joto akiwaonya watu wake wa karibu kupunguza kumshambulia Ruto.
Septemba 24, Gachagua alimtaka aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Laikipia, Cate Waruguru atulize makombora aliyokuwa akimrushia Ruto na washirika wake.
Mbunge huyo wa zamani, mmoja wa watu wa karibu na mtetezi wa Gachagua, alikuwa amemtembelea katika makazi yake huko Karen jijini Nairobi.
“Nafurahi kutembelewa na dada yangu mdogo. Napumzika hapa nyumbani na sijakwenda popote kwani siyo Ijumaa. Kesho, nitamwakilishi bosi wangu, Rais William Ruto katika ufunguzi wa Maonyesha ya Kimataifa ya Kilimo ya Nairobi kwa sababu yuko nje ya nchi,” alisema Gachagua kupitia video inayosambazwa mitandaoni.
Naye Waruguru akajibu: “Ni fahari yangu kukujulia hali na kukuhakishia kuwa Wakenya wamekusalimu na wanakupenda na wameniambia nipunguze maneno kidogo.
“Ndio, sasa punguza hizo, pale ulirusha kali zaidi. Hatupigani na yeyote. Sisi ni wapenda amani na hatuna shida na yoyote. Tutulie na tufanye kazi kwa Wakenya,” Gachagua akamwambia.
Akizungumza katika ibada ya Jumapili katika kanisa la PEFA eneo Bunge la Thika Mjini, mbunge huyo wa zamani alidai Ruto ndiye amewaagiza wabunge kuandaa hoja ya kumng’oa Gachagua.
“Rais wetu, ulisaidiwa na Mungu na sisi watu wa Mlima Kenya hadi ukaingia ofisi. Tuliadhibiwa vikali kwa kusimama na wewe sasa tunaona unataka kuadhibu Rigathi Gachagua na watu wa Mlima Kenya kwa sababu tumetofautiana na wewe. Hilo halitatendeka,” Waruguru alionya.