Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa serikali yake inataka amani, huku akionya pia kuwa iko tayari kupigana kwa kuwalinda raia wake. Ijumaa (28.09.2024 ) katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambayo ilisusiwa na baadhi ya wanadiplomasia ambao walitoka nje ya chumba hicho,Netanyahu amesema Israel maadui zao wanataka si tu kuwaangamiza, wanatafuta kuharibu ustaarabu wao wa kawaida, lakini pia wanatafuta kuirudisha dunia katika zama za giza za dhuluma na vitisho.
Katika hotuba yake, Netanyahu pia aliikosoa vikali Iran kwa kuhusika na mzozo huo wa Mashariki ya Kati. Huku akisema Israel ilikuwa inajilinda yenyewe dhidi ya Tehran katika nyanja saba.
“Tunashuhudia kipindi kibaya zaidi nchini Lebanon”
Umoja wa mataifa umesema Lebanon inapitia kipindi kibaya zaidi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili. Imran Riza, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Lebanon amesema machafuko ya hivi sasa hayana tofauti na janga. Riza amesema sekta ya afya ya Lebanon imezidiwa kabisa.
“Tunashuhudia kipindi kibaya zaidi nchini Lebanon katika kizazi na wengi walionyesha hofu yao kwamba huu ni mwanzo tu. Umoja wa Mataifa na washirika wake wanashirikiana kwa karibu na serikali ya Lebanon kuunga mkono juhudi za kukabiliana na hali hiyo. Hii ni pamoja na kuoanisha usambazaji wa misaada, kufanya tathmini ya pamoja, na kutambua mahitaji ya dharura kwa watu walioathirika.”, alisema Riza, akiwa nchini Lebanon.
Waasi wa Yemen wailenga Israel
Kwa upande wake, shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limelaani ongezeko kubwa la ghasia kati ya Israel na Hezbollah, likisema kwamba mashambulizi ya mabomu Lebanon yamewauwa watoto katika kiwango cha kutisha. Shirika la UNICEF limesema kati ya waliouwawa Jumatatu na Jumanne, hamsini walikuwa ni watoto.
Leo Ijumaa, Kundi la Hezzbollah lilirusha makombora katika miji ya Kirryat na Haifa kilomita 30 kutoka mpaka na Israeli na kwenye mji wa Tiberia. Jeshi la Israel lilitangaza kwamba liliyadungua makombora hayo.
Nao waasi wa Huthi wa Yemen wamesema walifanya shambulio la kombora na droni katika eneo la kati la Israel, baada ya jeshi la Israel kusema kwamba ulinzi wa anga ulinasa kombora lililorushwa kutoka Yemen.
Waziri wa afya wa Lebanon, Firass Abiad, alisema watu 25 wameuawa katika mashambulizi mapya ya Israel tangu alfajiri ya leo Ijumaa.
Vyanzo: AFP, Reuters, DPA