Mbeya. Baada ya kuanza na sare katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Championship, Mbeya City leo Ijumaa imetakata kwa kuinyoosha Mbeya Kwanza kwa bao 1-0.
Bao pekee la nyota na nahodha wa zamani wa Mbao FC, David Mwasa ndilo limetosha kuipa pointi tatu timu hiyo inayoshiriki ligi hiyo kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kushuka kutoka Ligi Kuu Bara.
Matokeo hayo yanaifanya Mbeya Kwanza ipoteze mechi ya pili mfululizo ikiwa ugenini baada ya awali kulala 2-1 mbele ya Songea United.
Kwa City hii ni mechi mbili mfululizo ikicheza nyumbani baada ya awali kutoka sare ya 2-2 na Bigman FC (zamani Mwadui).
Mwasa ameliambia Mwanaspoti kuwa, ushindi huo umetokana na masahihisho waliyofanya kufuatia mechi ya kwanza kukosa pointi tatu muhimu, akieleza kuwa kila mchezo kwao ni fainali.
“Wazoefu tupo wengi na tunajadiliana sana kuhakikisha timu inapata ushindi, tunaenda kujipanga tena na mchezo ujao ugenini tukiamini kocha atatupa mbinu kulingana na wapinzani walivyo,” amesema Mwasa.
Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Emmanuel Massawe amesema pamoja na yaliyojitokeza uwanjani kwa waamuzi, lakini wanakubali matokeo na wanarejea nyumbani, Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kwa mechi zijazo akiamini watasahihisha makosa.
“Ugenini ligi ni ngumu, kila timu inalazimisha matokeo ya ushindi, sisi pia tunaenda Nangwanda kuwapokea Cosmopolitan kisha Green Warriors tukihitaji pointi tatu kila mechi” amesema Massawe.