Mwijaku awasilisha mapingamizi  kesi ya Kipanya

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ndogo ya Dar es Salaam imepanga Oktoba 17, 2024 kusikiliza mapingamizi manne ya kisheria yaliyowasilishwa na mtangazaji wa Crown Media Ltd, Burton Mwemba Mwijaku,

Mwijaku amewasilisha mapingamizi hayo katika kesi ya madai iliyofunguliwa na mchora katuni maarufu, Ally Masoud Nyomwa maarufu kwa jina la Kipanya, akitakiwa kumlipa Sh5.5bilioni kwa madai ya kumkashifu kupitia mtandao wa kijamii.

Uamuzi huo umetolewa Septemba 26, 2024 na Jaji David Nguyale anayesikiza kesi hiyo, wakati shauri hili lilipotajwa kwa ajili ya Mwijaku kuwasilisha utetezi wake dhidi ya mlalamikaji.

Mahakama hiyo imepanga kusikiliza mapingamizi hayo siku hiyo saa 2:00 asubuhi kabla ya kuendelea na kesi ya msingi.

Mwijaku amewasilisha mapingamizi hayo kupitia kwa wakili wake, Gideon Opanda.

Katika mapingamizi hayo ya Mwijaku, yanahusu uwezo wa mahakama kusikiliza kesi hiyo, makosa ya uthibitishaji maelezo ya mdai, kukosekana usahihi wa vielelezo na kutozingatia kanuni za mwenendo wa mashitaka ya kashfa za mwaka 2019.

Mawakili watatu wanaomtetea Kipanya wakiongozwa na Alloyce Komba akishirikiana na Gerson Mosha na Rose-Shubi Mutakahwa, wamekubaliana na amri hiyo ya Mahakama ya kusikilizwa kwanza mapingamizi hayo, kabla ya kuendelea na kesi ya msingi.

Awali, kabla ya kuahirishwa kwa shauri hilo, mawakili wa Kipanya, waliomba mahakama ifute mapingamizi hayo kwa gharama zao kutokana na kasoro za kisheria walizobaini.

Jaji Nguyale baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17, 2024 kwa ajili ya kusikiliza mapingamizi hayo.

Katika kesi ya msingi, Kipanya amefungua kesi hiyo ya madai namba 18911 ya mwaka 2024, akiomba nafuu 12 ikiwemo kulipwa fidia kwa kukashifiwa mtandaoni na mwijaku.

Katika nafuu hizo 12, Masoud ambaye ni mtangazaji wa Clouds Media Group (CMG) anaomba alipwe fidia ya Sh5.5bilioni kutoka na Mwijaku kwa madai ya kumshushia hadhi na heshima yake kupitia mitandao ya kijamii.

Katika kesi ya msingi, Masoud amemshtaki Mwijaku kwa madai ya kumkashifu kwa maandishi Juni 4, 2024 kupitia kurasa zake za Facebook na Instagram, ambako anadaiwa kuandika maneno yenye nia ovu na kumfedhehesha, yakiwemo kwamba anafanya biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana wengi nchini.

Katika hati hiyo ya mashtaka, Mwijaku anadaiwa kuandika kwenye akaunti za mitandao tajwa kwamba Masoud huwazodoa na kuwadhalilisha viongozi wa nchi na Serikali hususani marais kwa kuhongwa.

Kipanya amedai kuwa maneno hayo ya uongo na yenye nia ovu yaliyochapishwa mitandaoni na kusomwa na watu wengi ndani ya jamii na duniani yametafsiri kwamba yeye  sio mtu mwenye tabia nzuri wa kupewa heshima yoyote kwani hafai, anajihusisha na biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za Serikali au magendo.

“Hivyo kipato chake kinatokana na biashara hiyo haramu na sio uchoraji katuni, utangazaji, ubunifu, ubalozi wa masuala ya kijamii, ukurugenzi wa bodi za taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa” ilidai sehemu ya hati ya mashtaka.

Kipanya, anaoimba mahakama iamuru Mwijaku kuomba radhi bila masharti yoyote na kuondoa mitandaoni maneno ya kashfa yaliyoandikwa na kusambazwa.

Lakini pia, Kipanya anaiomba mahakama itamke na kumuamuru Mwijaku, wakala wake, wasaidizi wake na mtu mwingine yeyote aliye katika mamlaka yake kutosambaza maneno hayo ya uongo na kashfa dhidi ya Masoud Kipaya.

Mbali na maombi hayo, Kipanya pia ameomba kulipwa gharama ya kesi kutokana na kuajiri mawakili na nafuu nyingine ambazo mahakama itaona ni haki na zinafaa apewe.

Related Posts