Nchi 9 kukutana Tanzania kujadili ubora wa elimu

Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la ubora wa elimu (IQEC), litakalowakutanisha wadau wa elimu zaidi ya 350 kutoka  nchi tisa za bara la Afrika.

Kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 12 hadi 14 litawakutanisha wadau wa elimu kutoka nchi za Zimbabwe, Zambia, Sudani Kusini, Lesotho, Afrika Kusini, Kenya, Rwanda, Uganda na mwenyeji Tanzania kupitia uratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).

Mratibu wa TENMET Martha Makalla amesema dhamira kuu ya kongamano hilo ni kuimarisha mifumo ya elimu nchini kulingana na mabadiliko ya haraka yanayoendelea duniani hasa yale ya kisayansi na kitekinolojia.

Martha ameeleza kuwa  kongamano hilo  litajikita  katika kuleta mawasilisho na mijadala inayoendana na mwelekeo wa sera na inayolenga kutoa utatuzi wa changamoto mbalimbali za kielimu nchini na barani Afrika.

Amesema kupitia kongamano hili Serikali, watunga sera, wanazuoni, wanafunzi, walimu, watafiti, mashirika ya umma na binafsi na asasi za kiraia hupata fursa ya kujadili hali ya ubora wa elimu kwa kubadilishana mawazo na uzoefu, kisha kujenga mikakati ya kuboresha utoaji wa elimu hapa nchini na kwingineko Afrika.

“Wadau takribani 350 wanaotekeleza afua za kuboresha elimu kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika watakutana nchini kujadili na kushirikishana mawazo, uzoefu huku wakitatua changamoto mbalimbali ili kuongeza tija na kuimarisha mustakabali wa elimu.

“Kongamano la mwaka huu limebebwa na kauli mbiu isemayo ‘Kukuza Mifumo ya Elimu Imara kwa Maendeleo Endelevu Barani Afrika’, ikilenga  kuhakikisha  mifumo ya elimu inajibu kwa ufanisi changamoto za sasa na kuwa na uwezo wa kuhimili mabadiliko yatokanayo na mapinduzi ya teknolojia ili kuhakikisha maendeleo endelevu na ya kudumu barani Afrika”amesema Martha.

Akizungumzia kongamano hilo Mshauri Mtafiti wa Hakielimu,  Dk Wilberfoce Meena anasema mikutano ya aina hiyo inapofanyika nchini inatoa nafasi kwa wadau kutafakari kuhusu ukuaji wa elimu na kubadilishana uzoefu na watu wa mataifa mengine.

“Ili tuweze kufanya maamuzi sahihi na bora kwa elimu yetu ni muhimu tufanye tukiwa na taarifa zinazotokana na tafiti za kisayansi hivyo naona kuna faida kubwa ya kuwa na mikutano na makongamano ya aina hii,”amesema Dk Meena.

Miongoni mwa mambo yatakayojadaliwa kwenye kongamano hilo ni mikakati ya kuimarisha mifumo ya elimu imara kwa mandeleo endelevu barani Afrika, mchango wa teknolojia katika kuboresha mifumo ya elimu na uendelezaji wa mbinu za kufundishia na kujifunzia kwa karne ya 21.

Mengine ni kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wote na kujenga mifumo ya elimu inayokabili changamoto za sasa, kubadilishana uzoefu kutoka ndani na nje ya Tanzania kuhusu jitihada na mafanikio katika sekta ya elimu, kusambaza matokeo ya utafiti kuhusu tafiti mbalimbali za elimu na mbinu bunifu za ugharimiaji wa elimu – mitazamo ya kimataifa na ya ndani.

Related Posts