Dodoma. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema wazazi ni mojawapo ya vyanzo vya watoto kuacha shule, kwani wengi wao huwaachia walimu jukumu la malezi.
Amesema katika kipindi hiki chenye wimbi la mmomonyoko wa maadili linaloikumba jamii, malezi ya wazazi kwa watoto ni muhimu.
Sangu ameyasema hayo leo Septemba 27, 2024 katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe wilayani Mpwapwa.
Amesema kitendo cha jumla ya wanafunzi 80 kuacha shule kati ya wanafunzi 247 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021 kutokana na sababu za utoro na mimba, ni ishara kuwa kuwa kuna baadhi ya wazazi hawawajibiki ipasavyo.
“Leo jumla ya watoto 157 wanahitimu kidato cha nne, huku tukiwa tumepoteza watoto 80 kutokana na tatizo la utoro na mimba za utotoni, hii sio sawa, wazazi angalieni hili,” amesema.
Ameongeza: “Elimu ndo msingi wa kila kitu ukiamua kuwa mfanyabiashara ni lazima uwe na elimu ukitaka kuwa mjasiriamali ni lazima uwe na elimu,’ amesisitiza Sangu
Pia Sangu amewataka wazazi kujiepusha na tabia ya kuwaozesha mabinti katika umri mdogo badala yake wahakikishe wanakumbatia elimu itakayowaandaa kwa ajili ya kupambana na maisha ya baadae
Katika hatua nyingine, Sangu amesema Serikali inatarajia kuwapangia vituo vya kazi jumla ya walimu 247 katika Mkoa wa Dodoma hususan katika Wilaya ya Mpwapwa, kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa walimu unaoikumba wilaya hiyo.
Amesema walimu hao watapelekwa katika wilaya mbalimbali ikiwemo Mpwapwa hivi karibuni ikiwa ni kati ya ajira 11,015 za walimu zilizokuwa zimetangazwa na Ofisi ya Rais, Sekretariet ya Ajira mwezi Julai mwaka huu.
Amesema Serikali imejipambanua kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora, ndio maana anafanya kila liwezekanalo kuhakikisha suala la uhaba wa walimu katika shule mbalimbali nchini linakuwa historia.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kibakwe, Mak Kalunguyeye amesema bado kuna mwamko mdogo wa elimu, kwani wazazi walio wengi wakishawapeleka watoto wao shule wanaona jukumu lao limekwisha.
“Wazazi wamekuwa wakiwatelekezea walimu watoto pale wanapokuwa wamewaleta shule, hiyo inafanya mwamko mdogo hata wanaporudi nyumbani hakuna wa kuwafuatilia,” amesema.