NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amewapongeza Wakazi wa Kitongoji cha Kiruwa kilichopo Kijiji cha Ruvu Mbuyuni Kata ya Mabilioni kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye sekta ya Elimu kwa kujitoa kwa hali na mali kuibua ujenzi wa vyumba viwili na Ofisi za Walimu kwenye Shule ya mpya ya Msingi Kiruwa.
Kasilda ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kisha kusikiliza na kutatua kero na malalamiko ya wanachi, ambapo amesisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na Wananchi hao kinapaswa kuigwa kwa vitendo kwani Serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu kwa wakati mmoja bali inahitaji ushirikiano kutoka kwa Wananchi na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma muhimu kwenye jamii zinapatikana.
“Serikali imesha agiza nyinyi mjenge mpaka ngazi ya Renta mkifika hapo sasa mnaanza kudai, kwahiyo kwasababu Mkurugenzi amekili ameona kazi nzuri mtendaji sasa iingize kwenye bajeti na mimi nitaongeza nguvu ili fedha zije hapa”. Alisema Kasilda.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Mbuyuni Vicent Mchomvu amesema Ujenzi wa mradi wa Shule hiyo ulianza mwaka 2019 kwa nguvu za Wananchi ukiwa na thamani ya Shilingi Milioni kumi na saba na laki tatu hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi Milioni kumi na tatu na laki tano (13.5), ujenzi bado unaendelea kufikia ngazi ya lenta ambapo Serikali nayo itakuja kumalizia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ili kuhakikisha mradi unatoa huduma kwenye jamii husika kama ilivyokusudiwa.
Naye Katibu mwenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya hiyo Mohamed Ifanda amesema hayo yote yanayofanywa ikiwemo juhudi za wananchi na Serikali ni sehemu ya kuimarisha huduma muhimu kwenye jamii kama ilivyokuwa dhamira ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana karibu na jamii husika.