‘Boni Yai’ asogeza mbele uchaguzi Kanda ya Pwani

Dar es Salaam. Kitendo cha meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob ‘Boni Yai’ kuendelea kusalia mahabusu kimesababisha uchaguzi wa Kanda ya Pwani ya Chadema uliopangwa kufanyika Septemba 29, 2024 kusogezwa mbele.

Jacob ambaye ni mmoja wa wagombea wa uenyekiti wa kanda hiyo, jana Septemba 26, ilidhaniwa angepata dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako ameshitakiwa akikabiliwa na kesi ya uchapishaji wa taarifa za uongo kwenye mitandao, hata hivyo haikutolewa.

Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Jerry Kerenge uchaguzi huo utakaohusisha pia viongozi wa mabaraza ya vijana, wazee na wanawake ya chama hicho ulipangwa kufanyika Septemba 29 katika ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Tasuba) wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Kerenge amesema uchaguzi huo utajumuisha wagombea 34 na wapigakura 95 ndio watakaoamua hatima yao.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 27, Kerenge amesema kutokana na mgombea mmoja (Jacob) kuwa mahabusu wameamua kuusogeza mbele hadi Oktoba mosi, ndipo watatangaza tarehe ambayo uchaguzi utafanyika.

Mahakama jana Septemba 26 ilisikiliza ombi jipya la upande wa mashitaka la kuondoa ombi la awali la kuiomba Mahakama iamuru mshtakiwa kutoa nywila zake, wakidai waliwasilisha kimakosa kinyume cha sheria.

Awali, upande wa mashtaka uliwasilisha maombi mawili, ukiomba Mahakama iamuru atoe nywila (neno la siri) za simu zake na akaunti yake ya mtandao wake wa X (zamani twitter), ili vifanyiwe uchunguzi na mpelelezi.

Pia, uliomba Mahakama izue dhamana yake kwa madai ya usalama wake, ukidai maombi hayo yanatokana na kile mshtakiwa alichomweleza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Davis Msangi kuwa baada ya taarifa alizoandika anajua kuwa atatekwa na kuuawa. Uamuzi wa ombi la awali ulikuwa utolewe jana.

Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga aliahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba mosi kwa ajili ya uamuzi wa ombi jipya la Jamhuri.

Kutokana na hilo, Kerenge amesema, “ngoja tuone siku hiyo kutakuwa na ishu gani kuhusu mgombea huyu. Kufanya uchaguzi halafu mgombea mmoja yupo ndani (mahabusu), inawezekana hatumtendei haki, tumeamua tujipe muda kidogo.”

“Hizi ni siasa wakati mwingine unaweza ukafanya jambo kwa faida, lakini likatengeneza ugumu, tusubiri tarehe moja,” amesema.

Jacob katika uchaguzi huo atachuana na Gervas Lyenda ambaye ni Ofisa Habari wa Kanda ya Pwani inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza na Mwananchi, Lyenda amesema anaendelea vyema na kampeni za kusaka kura kwa wajumbe, akibainisha kwa namna alivyojipanga ataibuka kidedea katika uchaguzi huo.

“Vipaumbele vyangu ni kushinda vijiji, vitongoji, mitaa yote ya Kanda ya Pwani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu, nimejipanga vizuri nina uzoefu na chaguzi,” amesema.

Lyenda amesema vipaumbele vingine ni kuimarisha chama hicho, Kanda ya Pwani kwa kuhakikisha kinakuwa na nguvu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na hatimaye kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Lyenda ndio mtu sahihi kuiongoza Kanda ya Pwani, nina sifa na vigezo, pia nina historia ya uongozi nikiwa katibu wa wilaya ya Ilala,” amesema.

Lyenda amesema endapo ataibuka kidedea atahakikisha anaunganisha chama hicho na siyo kuwagawa wanachama, akijinasibu kwamba yeye ni mtu anayefahamika ndani ya Kanda ya Pwani.

Ernest Mgawe, meneja kampeni wa Jacob, amesema wanaendelea na kampeni za mgombea kupitia vikao mbalimbali vinavyofanyika kwa njia ya mtandao na kuonana ana kwa ana na wajumbe ili kuwashawishi wampigie kura.

“Kuna timu kadhaa tulizozigawanya katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kusaka kura za Boni Yai, kwa mwenendo tuliokuwa nao mambo yanakwenda vizuri, tuna uhakika tutaibuka washindi,” amesema.

Mgawe ambaye ni mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba, amesema Boni Yai ana vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuhakikisha Kanda ya Pwani inashinda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwenye mchakato utakaofanyika Novemba.

“Boni Yai akishinda uchaguzi huu, atahakikisha anaboresha ofisi za majimbo 19 ya Kanda ya Pwani, shughuli ambayo ameshaanza kuifanya, lakini pia atahakikisha anakuwa mstari wa mbele kusaidia kuimarisha chama, kuimarisha umoja na mshikamano,” amesema.

Kwa muda mrefu Kanda ya Pwani, imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Baraka Mwago, baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye aliyekuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kurejea CCM kushindwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 19, 2019.

Katika uchaguzi huo alikuwa mgombea pekee lakini akapigiwa kura ya hapana.

Related Posts