Tira yachagiza elimu ya bima kwa wananchi wote

Arusha. Watoa huduma za bima Kanda ya Kaskazini wametakiwa kutoa elimu zaidi juu ya bima kwa wananchi wanaowahudumia,  kwa sababu wengi wao hawana uelewa wa kutosha kuhusu maswala hayo.

Hayo yamesemwa leo Septemba 27, 2024 na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Kaskazini, Bahati Ogolla wakati akizungumza katika kikao kazi kilichowashirikisha watoa huduma wa bima kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Tanga).

Amesema lengo la kikao hicho ni kukutana na wadau hao na kuweza kujadili changamoto zinazowakabili ikiwamo kuzitafutia suluhu ili kukuza soko la bima.

Ogolla amewataka kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu hiyo katika makundi mbalimbali nchini ili kufikia shabaha ya asilimia 80 kwa mwaka 2030 ya Watanzania kuwa na uelewa wa bima na bidhaa zake.

“Nawaombeni sana mwongeze  bidii katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya bima kwani elimu bado haijatolewa vya kutosha na mpite pia  katika makundi ambayo hayajafikiwa vya kutosha ikiwemo migodini na vijijini ambapo bado wananchi wengi wana uhitaji wa bidhaa za bima na elimu yake,” amesema Ogolla.

Aidha, amewataka watoa huduma wote kutekeleza makubaliano yote yaliyotolewa katika kikao kazi hicho na kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kupata mrejesho.

Ameongeza kuwa, taasisi hio ya Serikali majukumu yake makubwa ni kusimamia soko la bima na kulinda haki za wateja na walaji wa bima.

Kwa upande wake,  Ofisa leseni na usajili kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), John Joseph amewataka wadau kuhakikisha wanakata bima sahihi kulingana na miongozo iliyotolewa na mamlaka ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kutokea.

Naye Meneja masoko kutoka kampuni ya bima ya Bumaco mkoani Kilimanjaro, Gasto Mrema amesema kuwa, wamekuwa wakipeleka elimu kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutafuta aina mpya ya soko ili kuhakikisha majanga hayatokei tena.

“Sisi tumekuwa tukitoa mikataba ya muda mfupi na mrefu, pamoja na kutoa elimu kuhusu uwekezaji, bima ya majengo, uwekezaji kwenye saccos (Ushirika wa kuweka na kukopa), ambapo tupo nchi nzima katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma,” amesema Mrema.

Related Posts