Rais Samia awapa wanafunzi mbinu ya kufaulu

Namtumbo. Rais Samia Suluhu Hassan amewapa wanafunzi mbinu ya kufaulu mitihani, akisema majibu ya maswali yote yanapatikana kupitia Teknonojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Amewataka wanafunzi kuikumbatia Tehama wawe na ujuzi kuhusu akili mnemba (AI).

Amesema hayo leo Septemba 27, 2024 baada ya kuzindua Shule ya Sekondari ya Dk Samia Suluhu Hassan maalumu kwa wasichana wilayani Namtumbo, akiwa ziarani mkoani Ruvuma.

 “Nataka niwaambie siri, mkijifunza (AI) majawabu yote yapo kwenye mitandao, yote ya masomo yenu, ukiingia kwenye Google, sijui ChatGPT, kote huko kuna majawabu yote mnayosomeshwa hapa, kwa hiyo mkitumia vizuri mtaweza kujifunza vizuri,” amesema.

Rais Samia amesema wanafunzi hawana budi kujifunza teknolojia hizo kwa kuwa ndiyo mwelekeo wa dunia, akisisitiza kwa kadri siku zinavyokwenda matumizi ya karatasi na kalamu yanapungua.

“Mambo mengi tutakuwa tunayafanya kwenye mitandao, kwa hiyo niwasisitize mtumie fursa hiyo kila mmoja wenu akitoka hapa awe fundi wa kutumia hayo mambo,” amesema.

Amesema sababu ya kujengwa shule hiyo na nyingine katika mikoa yote nchini ni kuhakikisha zinawashirikisha wanawake katika sanaa na sayansi.

Rais Samia amesisitiza ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inatekelezwa ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.

Amesema shule hiyo inatumika nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia, akisisitiza ni vema ifanywe hivyo kwa kila taasisi inayohudumia watu zaidi ya 100.

“Wanawake wa Afrika wanapata maradhi kwa sababu ya kupikia kuni, wanapata maradhi ya kupumua na wanapofua macho kwa sababu ya moshi, umefika wakati wa kubadilika kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema.

Rais Samia amewataka wanafunzi shuleni hapo kutumia vema nafasi waliyoipata, akiwasihi walimu kuwatunza watoto hao wasipate ujauzito.

“Sitaki nisikie kwenye shule hii kuna msururu wa waliopata sifuri, wamekosa vyeti sijui daraja la nne, mmenihakikishia kwenye kufaulu hakuna shida, sasa hilo ndilo nataka kusikia,” amesema.

Amesema ameridhishwa na mwamko wa wazazi mkoani Ruvuma kuandikisha wanafunzi wa elimu ya awali na msingi mwaka huu.

Samia amesema wanafunzi 49,396 wa elimu ya awali waliandikishwa mwaka huu mkoani humo, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 7,256 ukilinganisha na mwaka 2023.

Kwa darasa la kwanza amesema wanafunzi 52,636 wameandikishwa ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 7,775 kulinganisha na mwaka jana.

Amesema Serikali imefikisha huduma kadhaa mkoani humo, ikiwemo ya maji, akieleza katika kila wananchi 10 watatu wamefikiwa na maji.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh4.6 bilioni.

Amesema shule hiyo ni moja kati ya 26 zinazoendelea kujengwa katika kila mkoa nchini, kwa ajili ya wasichana kwa mchepuo wa sayansi na sanaa. Wanafunzi 4,843 wameshaanza masomo katika shule zilizokamilika kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Kwa niaba ya wanafunzi shuleni hapo, Stella Magao amesema licha ya shule hiyo kuwa mbali na mji, hawakuwahi kushuhudia viashiria vya uvunjifu au upotevu wa amani.

Amesema wanafunzi wote shuleni hapo wamepata bima za afya kwa gharama nafuu na wamepwa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira.

Amemuomba Rais awapatie gari la shule, ombi ambalo Samia amejibu kuwa usafiri huo upo njiani.

Pia, wameomba kuongezwa walimu kwa kadri wanafunzi watakavyoongezeka, akieleza waliopo sasa wanatosheleza kulingana na idadi ya wanafunzi.

Related Posts