Mama anayedaiwa kuuawa na mwanawe akigombea mali azikwa

Moshi. Wakati mamia ya wananchi wakijitokeza kumzika Adela Mushi (74), mkazi wa Kijiji cha Okaseni, wilayani Moshi anayedaiwa kuuawa na mwanawe wakigombea mali, Paroko wa Parokia ya Mawela, Patrick Soka amesema asilimia 60 ya migogoro iliyopo kijiji hapo ni ya ardhi na urithi.

Amesema migogoro hiyo imekuwa ikichochea ukatili yakiwemo mauaji kwenye familia. Padri Soka amesema hayo leo Septemba 27, 2024 akiongoza ibada ya mazishi ya mama huyo.

Katika mahubiri amesema kila mara wamekuwa wakisuluhisha migogoro ya ardhi na nyumba za urithi, hivyo akaitaka jamii kuridhika na mali walizonazo na kuacha kugombana katika familia.

Adela aliyezikwa kwenye makaburi ya familia yaliyopo kijijini hapo, anadaiwa kuuawa Septemba 23 na mwanaye mwenye umri wa miaka 54 kwa kumyonga kwa kutumia kipande cha kanga na kisha kumkata na shoka usoni. Mwili wake ulitelekezwa chumbani kwake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa muda mrefu wa kugombea mashamba na mali za marehemu.

Alisema wanamshikilia Nemes Dominick kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Akitoa mahubiri, Padri Soka amesema: “Ni lazima kama jamii tujitathmini na kujitafakari katika kijiji hiki, ulevi umekuwa ni changamoto kubwa, uhusiano mwingi katika baadhi ya familia ni mbaya na hasa unaohusu ardhi na nyumba za urithi.”

“Kila mahali tunapokwenda kwenye mitaa yote kitu kinachochukua muda mwingi kusuluhisha ni migogoro inayotokana na matatizo ya ardhi, sasa tumefikia wapi huku sisi watoto wa kizazi hiki? tujirekebishe ndugu zangu, haya mambo ya ardhi yatakuwepo tu, ridhikeni na maeneo mnayopewa,” amesema.

Jeneza lenye mwili wa Adela Mushi (74) anayedaiwa kuuliwa na mwanaye mwenye umri wa miaka 54 likiingizwa kabirini, nyumbani kwako Okaseni Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.Picha na Omben Daniel

Kuhusu ulevi amesema; “Lazima tujishauri ndugu zangu kwamba ulevi haulipi, hivyo tujitafakari sana. Changamoto nyingine ni ukatili ndani ya familia, ni kitu cha kumlilia Mungu lakini tukifanyie kazi, uhusiano wa wazazi na watoto, ndugu kwa ndugu, mume na mke ni lazima tufanye bidii turekebishe uhusiano wetu,” amesema.

Akisoma historia ya marehemu, mjukuu wa mama huyo, Innocent Mushi, amesema kifo cha bibi yao kimewaumiza na ameacha pengo lisilozibika katika familia yao.

Amesema alikuwa na upendo kwa familia na ndiye aliyekuwa mshauri.

Amesema bibi yao ana watoto sita, wajukuu 36 na vitukuu watatu.

Related Posts