Hekaya za mlevi: Kijana elimu haijakufunza kuajiriwa

Dar es Salaam, Kuna wakati kila kijana alitamani kuwa msanii. Hii inatokea baada ya akili ya kijana kumwonesha mjomba wake akisota na shahada zake bila kupata kazi. Lakini pia masikio ya kijana yaliwanasa wale waliopata kazi wakalalamikia hali ngumu ya maisha.

 Kwa upande wa pili kijana aliwaona na kuwasikia vijana wasanii wakijigamba na majumba na magari ya kifahari. Wakiyaponda maisha hadi kusahau kuwa kufa kwaja.

Wengi wa vijana hawa walikuwa wakifeli kila walipojaribu kuingia kwenye sanaa. Mtu anaamini kabisa kuwa ana uwezo hasa baada ya kusifiwa na wenzake. Lakini kila akienda kujaribu bahati yake anaangukia pua baada ya kuonekana hana uwezo.
 

Anabaki akilaumu kwamba kila penye sanaa hapakosi fitna. Mwisho anaamini kuwa mafanikio anayoyaona kwa wasanii hayawezekani bila kujulikana, milungula au ndumba. 

Lakini vijana wachache waliobahatika kuingia kwenye ulingo wa sanaa waligundua mambo tofauti kabisa. Sanaa ni kazi sawa na kazi zingine kadiri unavyojibidiisha ndivyo unavyokula.

 Huko hakuna kulala, saa nane za usiku wakati wenzio wanakoroma wewe unapiga kazi. Mchana badala ya kupumzika unatakiwa kufanya mazoezi. Ukilala utakula ugali kwa picha ya samaki, yaani utajiposti mbele ya Range Rover wakati unakopa hela ya kurikwesti usafiri. 

Kosa la vijana wetu ni kuyaona mafanikio kabla ya kuijua kazi yenyewe. Na hili naliona kwa wale wanaozurura na vyeti wakilalamika ukosefu wa ajira. Mtu anamaliza vyuo bila kujua namna ya kutengeneza ajira.

Na akipata mwanya wa ajira, anaweza kusaini mkataba bila kuusoma ili akalalamike tena.Wanadhani ukubwa wa shahada zao ndiyo tiketi ya mafanikio.

Wakati fulani kila mmoja wetu aliamini kuwa watu waliokosa uwezo darasani ndio waliopelekwa vyuo vya ualimu. Lakini kumbe mtu aliweza kufanya vizuri kwenye masomo yake, ila akafeli kuchagua muunganiko wa masomo ambayo yangempeleka chuoni. 

Hii inatosha kumwonesha kijana wa sasa kuwa hakuna kazi isiyohitaji elimu. Hata wakulima, wawindaji na wavuvi wasiojua darasa wana elimu ya mapokeo kutoka kwa mababu.

Ukitaka kuamini rejea mifano ya sanaa ya pale mwanzo. Vijana wanapotaka mafanikio kama ya msanii fulani, ni lazima waelewe kuwa huyo asingelikuwa vile bila ya mafundi wanaomfanya awe vile aonekanavyo. Nyuma ya msanii kuna waandishi wa kazi za sanaa, wahariri, waongozaji, wapiga picha, wazalishaji, watangazaji na wasambazaji. Hao ndio wasanii.

Kiujumla elimu ni ujuzi wa kutumia vipawa kama fursa. Mtu aliyezaliwa mashambani atajua kulima, atajifunza kuugeuza utamaduni wake kuwa shughuli ya kumpatia kipato. Kwa mfano mkulima atauza sehemu ya mazao yake ili kujipatia mahitaji mengine muhimu kama mavazi, dawa n.k.
 

Kadhalika yule aliyekulia mwituni atakuwa mwindaji, aliyeishi kando ya ziwa naye atarithi utamaduni wa wavuvi.  
Lakini kwa kuwa utamaduni ni jambo mtambuka, mtu huyohuyo anaweza kuwa mhunzi. Anaweza kufua majembe, mapanga, nyengo na mishale akawauzia wakulima na wawindaji.

 Kumbe hata anayeishi ziwani anaweza kuwa msuka nyavu na madema, au kuwa muuza samaki badala ya kuwa mvuvi. Hata akina Neil Amstrong wasingeliweza kuweka historia ya kukanyaga mwezini bila wataalamu wa anga na wajenzi wa Apollo 11.

Mawazo ya kupata kitonga baada ya kusoma sana ni ya kizamani sana. Wakati ule baada ya uhuru walihitajika sana vijana wa kuchukua nafasi zilizoachwa na wakoloni. Kwa kuwa wakoloni waliwanyima elimu wazalendo kwa makusudi, baada ya uhuru hakukuwa na dira madhubuti miongoni mwa wazawa.
 

Ni wachache sana waliobahatika kusoma katika shule za wakoloni. Hivyo Serikali ilikuwa tayari kuwasomesha vijana wake ili waje kuisaidia nchi.

Walipohitimu, vijana hao waliajiriwa na kuwekewa mazingira mazuri kama nyumba za kuishi, usafiri, matibabu yao pamoja na familia na kadhalika. Japokuwa mishahara yao haikuwa mikubwa kivile, lakini walizila mbivu.

Ajabu kijana wa kileo anaota maisha yanayofanana na hayo ati kwa kulinganisha shahada zake na za wazee wale pengine hawaelewi au wanajizima data kwa makusudi.

Ulimwengu wa sasa ni tofauti na wa kale. Wakati ule mtu aliyeishia darasa la pili angeweza kuwa tarishi kwenye ofisi ya Serikali. Hivi sasa baada ya mapinduzi ya teknolojia, hakuna tena nafasi ya mesenja kwani barua hutumwa kielektroniki na vifurushi huletwa na kampuni zilizosajiliwa. Wafanyakazi wanapunguzwa kupisha mitambo ili kupunguza gharama na kupata ufanisi wa hali ya juu kazini.

Hizi ngonjera za kuingiza wahitimu zaidi ya laki sita kwenye nafasi elfu hamsini za ajira zinafaa kukomeshwa mara moja. Watoto wafundishwe masomo watakayoingia nayo mtaani badala ya kuzurura na vyeti. Waambiwe wazi kuwa tatizo la ajira ni la kidunia, hivyo wafute ndoto za kuajiriwa nje. 

Huko wanakokuwazia tayari kumeshaingia hapa nchini kutafuta hicho wanachokitafuta kwao.Ni muhimu kijana ajue anasoma ili awe nani, au asomee nini ili awe mtu wa ndoto zake. Nawafagilia wale wanaojigundua na kuifanya elimu kama nyenzo ya kujipata. 
 

Related Posts