MCT yapata rais mpya | Mwananchi

Dar es Salaam. Jaji Mstaafu Bernad Luanda amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), kwa kura 27 kati ya 29 zilizopigwa katika mkutano mkuu wa 26 wa wanachama wa taasisi hiyo.

Jaji Luanda atatumikia majukumu hayo katika nafasi hiyo akirithi mikoba ya Jaji Juxon Mlay aliyefariki dunia mwaka huu akiwa nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu, kutokana changamoto za kiafya zilizokuwa zinamkabili. 

Jina la Jaji Luanda lilifikishwa kwenye mkutano huo kwa ajili ya kupigiwa kura na wajumbe hao baada ya kupitishwa na bodi ya baraza hilo inayoundwa na Jaji Robert Makaramba, Dk Joyce Bazira na Nancy Angulo kama mtaalamu huru kutoka nje ya bodi hiyo.

Kwa mujibu wa Katiba ya baraza hilo, rais huyo atangoza mihula miwili ya kipindi cha miaka mitatu mitatu (kwa maana ya miaka sita).

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Leo Septemba 27, 2024 makao makuu ya MCT  Tegeta Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo, Nicholaus Mwaibale amesema Jaji Luanda amechaguliwa kwa asilimia 98.

“Kura zilizopigwa zilikuwa 29, kura mbili ziliharibika hivyo kwa mamlaka niliyopewa namtangaza Jaji Mstaafu   Luanda kuwa Rais mpya wa Baraza la Habari Tanzania (MCT),” amesema Mwaibale ambaye ni mfanyakazi wa Kituo cha Redio UFR-Tabora.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya za Habari za Maendeleo Zanzibar,(WAHAMAZA), Jabir Idrissa amekubalina na kiongozi huyo hasa timu iliyofanya mchujo wa majina anaiamini.

“Jina la mtu waliyempendekeza na kutuletea tunamuamini kutokana na rekodi zake nzuri katika muhimili wa mahakama ya uchapaji kazi,” amesema Idrissa amesema anamfahamu tangu akiwa hakimu kwenye mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu Dar es Salaam wakati akiripoti habari alitulia hasa katika kufanya maamuzi hivyo matumaini yake taasisi hiyo itapiga hatua.     

Licha ya kumpata kiongozi huyo, Mwenyekiti wa kikao hicho, Yussuf Khamis Yussuf amewataka wajumbe hao kufikiria upya kuona haja ya kufanya mabadiliko ya katiba yao iliyotengenezwa miaka 30 iliyopita.

“Katiba yetu ina upungufu mwingi ikiwemo rais akifariki duniani akiwa madarakani haisemi chochote, tunapaswa kubadilika na kufanya mabadiliko ili inapojitokeza kuwepo na njia ya kufanya,” amesema.

Related Posts