New York. Tanzania imeweka wazi msimamo wake kimataifa juu ya kupinga ukoloni mamboleo na vikwazo vya kiuchumi vinavyowekwa dhidi ya nchi zinazoendelea.
Sambamba na hilo, imesisitiza umuhimu wa ulimwengu kudumisha amani kuheshimu kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kushirikiana ili kufikia mustakabali mzuri na shirikishi.
Msimamo huo wa Tanzania, umetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana Ijumaa Septemba 27, 2024 alipohutubia mkutano wa 79 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) nchini Marekani, kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Ameijenga hoja hiyo kwa kurejea maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisema; “Tanzania siku zote imepinga ukoloni, ubaguzi wa rangi na aina zote za ukandamizaji.”
Katika hilo, ameisihi jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo vya kiuchumi vinavyozikandamiza nchi zinazoendelea chini ya ukoloni mamboleo.
Ameitaka moja ya nchi inayopitia magumu hayo ni Cuba, akisisitiza haki ya nchi hiyo na nyingine kujitawala na kufikia ustawi wa kiuchumi.
Katika hotuba yake hiyo, Majaliwa ameeleza msimamo wa muda mrefu wa Tanzania katika kulinda na kudumisha amani na ulinzi.
Aidha, ametangaza mipango ya Tanzania ya kuandaa Mkutano wa Nishati wa Afrika Januari 2025, jukwaa litakaloharakisha upatikanaji wa nishati safi barani humo.
Majaliwa ameunganisha mkutano huo na lengo la Tanzania kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira, jambo alilosema linaathiri afya na uendelevu wa mazingira barani Afrika.
“Safari yetu kuelekea maendeleo endelevu haikosi changamoto zake,” Majaliwa amesema, akirejelea athari za janga la COVID-19, majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na umaskini.
Hata hivyo, ameonyesha matumaini, akisisitiza uwekezaji wa kimkakati katika kilimo, nishati safi na teknolojia kama nguzo muhimu za ukuaji wa uchumi.
Katika hotuba hiyo, Waziri Mkuu, amewataka viongozi wa dunia kuchukua hatua za kuhakikisha faida za maendeleo zinawafikia wote.
Majaliwa amebainisha ni asilimia 17 pekee ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyokuwa kwenye mwelekeo sahihi kufikia mwaka 2023, akisisitiza ushirikiano wa kimataifa ili kuvunja vikwazo vya ukosefu wa usawa, pengo la kijinsia na mabadiliko ya tabianchi.
“Tanzania iko tayari kushirikiana na washirika wa kimataifa katika kusukuma mbele malengo haya,” amesema, akitaja mafanikio ya miradi mbalimbali nchini ikiwemo mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) na uwezeshaji wa wanawake kupitia kilimo cha mwani visiwani Zanzibar.
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Majaliwa amesisitiza umuhimu wa hatua za dharura, kwani Tanzania, kama nchi nyingi zinazoendelea, inakabiliana moja kwa moja na athari hizo ukiwemo ukame, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari.
Waziri Mkuu ametoa wito wa uwekezaji zaidi katika fedha za kuziwezesha nchi zinazoendelea kulikabili janga hilo, ili kujikwamua na kukabiliana na athari hizo.
“Ni muhimu, dunia iungane katika vita hivi ili kulinda vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.