Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Jamii, wazazi, na walezi wameaswa kujenga tabia ya kusema na watoto na kushiriki kikamilifu, katika malezi ya vijana kwa kuwapa mafunzo sahihi kabla hawajaathiriwa na mienendo mibaya inayoweza kusababisha mmomonyoko wa maadili.
Hatua hii ni muhimu ili kuwalinda watoto kwa ajili ya kizazi kijacho kilicho na maadili mema ya mtoto wa Kitanzania.
Wito huu umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Pius Lutumo, wakati akizindua kampeni ya “TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIWA” kimkoa, katika Viwanja vya Polisi, Chalinze.
Kamanda Lutumo alieleza, lengo kuu la kampeni hiyo ni kuhamasisha wanafunzi na vijana kuepuka tabia mbaya wanapokutana na mazingira mapya, hususan wanafunzi wa kidato cha kwanza, kidato cha tano, na wanavyuo wa mwaka wa kwanza.
“Kundi hili linaweza kujitambua na kuelewa athari za kuiga tabia mpya zinazoenda kinyume na maadili waliyojengewa awali,” alisema Kamanda Lutumo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Michael Manumbu, alisisitiza kuwa jukumu la kuwalinda watoto ni la jamii nzima.
“Watoto wanaolindwa ni sehemu ya jamii nzima, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha tunawaambia kabla hawajaharibiwa,” aliongeza.
Manumbu pia alibainisha kuwa matarajio ya kampeni hiyo ni kufikia shule 139 na vyuo vya kati 16 mkoani Pwani, ambapo jumla ya wanafunzi 12,927 na wanavyuo 1,968 wanatarajiwa kufikiwa.