Dar es Salaam. Kama wewe ni mnywaji wa pombe zinazotengenezwa kwa ngano au pombe kali, soma hapa kwa makini.
Wataalamu wa afya wameeleza uwepo wa athari hasi, kwa wale wenye tabia za kunywa pombe kabla ya kula chakula kwani huchangia mnywaji kula chakula kidogo kuliko mahitaji ya mwili au kuharibu kuta za utumbo.
Mtaalamu wa Lishe na Meneja Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Shirika la World Vision, Dk Daudi Gambo amesema athari inategemea ni pombe ipi amekunywa, kwani kuna tofauti kati ya pombe kali na zile zilizotengenezwa kwa ngano.
“Pombe zenye ngano kama bia aina zote, yule mtu anakuwa amechukua kaloris nyingi kutoka kwenye kabohaidreti, kwa maana hiyo anaweza kujikuta ameshiba na ile hamu ya kula chakula ikapungua kwa sababu nguvu tayari anazo, hivyo atapunguza nafasi ya yeye kula kitu kingine,” anasema.
Dk Gambo anasema mnywaji atakuwa amechukua kaloris, hivyo vitamin, protini, madini vyote hivyo amevikosa na wengi akishiba anaweza asile, hivyo hajapata virutubisho vyote vinavyopatikana kwenye makundi sita ya vyakula.
Anasema anayekunywa bia anakuwa amechukua sehemu moja na ameacha virutubisho kutoka makundi mengine na akishakunywa hamu ya chakula inapungua au inaisha kabisa.
Akizungumzia pombe kali, Dk Gambo anasema zinaathiri vimeng’enya chakula ‘enzymes’ na ikiathiri utengenezaji wa vimeng’enya chakula inaua wale wadudu waliopo kwenye utumbo.
“Pombe kali huingilia utengenezaji wa vitamin B zilizo muhimu kwa ajili ya wadudu wa tumboni na wale wanaohusika katika kumeng’enya chakula, hivyo kwa sababu ule mmeng’enyo wa utumbo unakuwa umepungua ndiyo maana wanaotumia pombe kali wanapata shida kama ya utapiamlo.
“Endapo amezidisha pombe, wale wadudu rafiki wanaosaidia mmeng’enyo wa chakula wanaotakiwa kutengeneza vitamin B kwenye utumbo mdogo wanapotea na ile simenti ya kwenye utumbo nayo inapata shida,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa afya ya jamii na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk Ali Mzige anasema ili watu waendelee kuwa na afya bora ni vizuri wale chakula saa 2 hadi 3 kabla ya kulala ili kutoa nafasi ya umeng’enyaji, pia uzungukaji wa damu mwilini, hususan kwenye ubongo, figo na moyo.
“Mtu anapokula chakula baada ya saa 2 usiku ni rahisi kurundika chakula katika eneo lake na kushindwa kutoa nafasi kwa mzunguko wa damu kwenda taratibu na wakati mwingine kusinzia,” anasema Dk Mzige.
Akitoa mfano, anasema kuna mtu mmoja alipoandaa sherehe ya binti yake, walipotoka kanisani walifikia kula ikiwa ni saa 12 jioni na baada ya hapo utaratibu mwingine ulifuata.
“Inawezekana tamaduni za nje zilikuwa zimemkaa hivyo alipofika huku akaamua kuendelea nazo na watu walimsifu kwa sababu baada ya sherehe, waalikwa walikuwa na nafasi ya kufanya vitu vingine bila kuathiri afya zao ambazo zingesababishwa na chakula,” anasema.
Dk Mzige anasema haipaswi mtu kunywa pombe kabla ya kula kwenye sherehe na kula chakula kingi kupita kiasi kwa usiku, kwani unywaji wa pombe unakwenda kuchukua nafasi ya chakula na kusababisha kuwa cha ziada.
Anasema inapotokea kwenye sherehe wameanza kula, haitakiwi kula kila chakula kilichopo, bali inatakiwa kuchagua vyakula vichache ambavyo uwezekano wa kumaliza upo na si kula mtu avimbiwe.
“Katika masuala ya ulaji mtu anatakiwa kula kidogo, siyo mtu anachanganya kipande cha kuku na samaki, wali, ndizi, pilau na vingine kwa wakati mmoja, kinachotakiwa ni kuchagua kimojawapo,” anasema Dk Mzige.
Hata hivyo, anasema cha kuzingatiwa kwenye sherehe wakati wa ulaji ni kutumia mboga za majani na matunda, ambapo inasaidia kupunguza saratani na tafiti zimefanyika takribani watu milioni 2 wanakufa kila mwaka kwa kutokula matunda na mboga za majani.
Mhudumu wa chakula katika sherehe, Mwatanga Madoda anasema ulajiwa chakula unacheleweshwa na wenye shughuli kwa kuingia ukumbini saa tatu tofauti na muda uliopangwa kwenye ratiba.