KONGAMANO LA NNE LA ELIMU BORA KIMATAIFA KUFANYIKA NOVEMBA 12, 2024 DAR

 

 

Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusiana na Kongamano la Kimataifa la Elimu Bora linalotarajia kufanyika Novemba 12 hadi 14, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).  Kulia ni Mshauri mwelekezi kutoka HakiElimu, Dk. Wilberforce Meena na Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Elimu Christian Social Services Commission, Makoye Japhet.


Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala (kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusiana na Kongamano la Kimataifa la Elimu Bora linalotarajia kufanyika Novemba 12 hadi 14, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).  Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Elimu Christian Social Services Commission, Makoye Japhet.


Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusiana na Kongamano la Kimataifa la Elimu Bora linalotarajia kufanyika Novemba 12 hadi 14, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).  Kulia ni Mshauri mwelekezi kutoka HakiElimu, Dk. Wilberforce Meena na Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Elimu Christian Social Services Commission, Makoye Japhet.

KONGAMANO la Kimataifa la Elimu Bora linatarajia kufanyika Novemba 12 hadi 14, 2024 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC). 

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala amesema kongamano hilo la elimu mwaka huu linatarajia kuleta pamoja wadau toka serikalini, watunga sera, wanazuoni, wanafunzi, waalimu, watafiti, mashirika ya umma na binafsi na asasi za kiraia.

Alisema wadau hao watapata fursa ya kujadili hali ya ubora wa elimu kwa kubadilishana mawazo na uzoefu, kisha kujenga mikakati ya kuboresha utoaji wa elimu hapa nchini na kwingineko Afrika. Dhamira kuu ni kuimarisha mifumo ya elimu nchini kulingana na mabadiliko ya haraka yanayoendelea duniani hasa yale ya kisayansi na kitekinolojia.

Bi. Makala alibainisha kuwa wadau takribani 350 wanaotekeleza afua za kuboresha elimu kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika wanatarajia kushiriki pamoja na kushirikishana mawazo, uzoefu huku wakitatua changamoto mbalimbali ili kuongeza tija na kuimarisha mustakabali wa elimu. 

Aidha alizitaja nchi zinazotarajia kushirikia katika mkutano huo ni pamoja na Zimbabwe, Zambia, Sudani Kusini, Lesotho, Afrika Kusini, Kenya, Rwanda, Uganda pamoja na Tanzania ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo.

“Tunatarajia pia wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Wizara za Elimu za nchi hizi kushiriki, wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wabunge. Pia kongamano hili litajikita hasa katika kuleta mawasilisho na mijadala inayoendana na mwelekeo wa sera na inayolenga kutoa utatuzi wa changamoto mbalimbali za kielimu nchini na barani Afrika.

“…Kongamano la mwaka huu limebebwa na kauli mbiu isemayo “Kukuza Mifumo ya Elimu Imara kwa Maendeleo Endelevu Barani Afrika” (Fostering Resilient Education Systems for Sustainable Development in Africa) kauli mbiu hi inalenga kuhakikisha kuwa mifumo ya elimu inajibu kwa ufanisi changamoto za sasa na kuwa na uwezo wa kuhimili mabadiliko yatokanayo na mapinduzi ya teknolojia ili kuhakikisha maendeleo endelevu na ya kudumu barani Afrika.”

Mratibu huyo wa Taifa wa TEN/MET, amezitaja miongoni mwa mada zinazotarajia kujadiliwa ni pamoja na Mikakati ya Kuimarisha Mifumo ya Elimu Imara kwa Maendeleo Endelevu Barani Africa,  Mikakati ya kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wote na kujenga mifumo ya elimu, inayokabili changamoto za sasa, Mchango wa Teknolojia katika Kuboresha Mifumo ya Elimu, Uendelezaji wa Mbinu za Kufundishia na Kujifunzia kwa Karne ya 21.

Aliongeza kuwa nyingine ni Kubadilishana Uzoefu kutoka ndani na nje ya Tanzania kuhusu jitihada na mafanikio katika sekta ya elimu, Kusambaza Matokeo ya Utafiti kuhusu Tafiti Mbali Mbali za Elimu, Mbinu Bunifu za Ugharimiaji wa Elimu – Mitazamo ya Kimataifa na ya Ndani na Maonesho ya juhudi za Wadau wa Elimu, kupitia utekelezaji wa afua mbalimbali, na kazi za kibunifu zinazofanywa katika sekta ya elimu na jinsi zinavyosaidia kuimarisha mifumo ya elimu.

Kongamano la mwaka huu linaandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo; Christian Social Services Commission (CSSC), CAMFED, Msichana Initiative Organization, PESTALOZZI Children Foundation, Shule Direct, Plan International, Save the Children, UWEZO Tanzania, African Child Projects, HakiElimu, Policy Forum, UNHCR, Agakhan Foundation, Flaviana Matata Foundation na Tai Tanzania.

Related Posts