Polisi yanasa mtandao wa mauaji Dodoma

Dodoma. Watu wanne wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika mtandao wa mauaji jijini Dodoma.

Wanatuhumiwa kusababisha vifo vya watu wanane, huku watano wakijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Waliokamatwa katika mtandao huo unaodaiwa kuhusika katika matukio manne ya mauaji yaliyotokea kati ya Julai mosi na Septemba 16, 2024 ni wakulima wanne wakazi wa Mtumba, jijini Dodoma.

Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa jana Septemba 27 imewataja watuhumiwa hao kuwa ni Paulo Mwaluko (22), Isack Richard (24), Ernest Richard (24) na Silvanus Shotoo (21).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi katika taarifa hiyo amesema uchunguzi umebaini katika matukio hayo yote watuhumiwa wamekuwa wakiwapiga watu kwa kitu kizito wanaowakuta kwenye nyumba walizovamia.

Amesema baada ya hapo, huwafanyia vitendo vya udhalilishaji na kisha kuchoma moto ili ionekane ni shoti ya umeme imetokea.

“Uchunguzi zaidi unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria zifuate. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linapenda kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao uliofanikisha kukamatwa kwa mtandao wa mauaji,” amesema.

Akizungumza na waandishi wa habari alipotoa taarifa hivyo, Kamanda Katabazi amesema mtandao wa mauaji yaliyojitokea jijini Dodoma hivi karibuni wameuvunja na watuhumiwa wote wamewakamata.

Amesema kinachosubiriwa ni hatua nyingine za kisheria zikamilike ili wafikishwe mahakamani.

“Kila watuhumiwa wana namna ya kutenda uhalifu. Ni kikundi ambacho almost (takribani) ni watu walewale wanarudia na kuongezeka. Kijumla ni kikundi cha aina moja kinachohusika,” amesema.

Katabazi amesema watuhumiwa hawakutumwa na mtu ila ni kikundi cha mauaji ambacho kinalenga kujipatia mali.

“Ni ukiukwaji wa maadili, lengo ni kuwania mali. Hata walipokwenda kule (katika matukio) walikuwa na nia ya kujipatia fedha. Wakiingia (katika nyumba) wanaangalia kama kuna fedha wanachukua na mali nyingine. Kwa hiyo siyo kikundi ambacho kimetumwa ni kuwania mali,” amesema.

Amesema kwa matukio yote manne vyanzo ni kuwania mali na mmomonyoko wa maadili kwa sababu vitendo vinavyofanyika ni vya kikatili na si vya kibinadamu.

Katabazi amedai watuhumiwa hao walihusika katika tukio la Julai mosi, 2024 eneo la Mahomanyika Nzuguni jijini Dodoma ambako Maria Thomas (20) na Maria Timothy (22) waliuawa usiku katika grosari waliyokuwa wakifanya kazi kisha miili yao kuchomwa moto.

Katika tukio hilo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilisema ni moto wa hujuma kwa sababu milango ya nyumba ilikutwa imefungwa kwa nje, mwili mmoja ulikutwa umefungwa mikono kwa nyuma kwa kutumia kitenge, huku mwingine akijeruhiwa maeneo ya kichwa.

Tukio lingine lililotokea Agosti 28, 2024 eneo la Mbuyuni Kizota ambako aliuawa Michael Richard (36) kwa kupigwa na watu wasiojulikana na kisha kuchomwa moto godoro alilokuwa amelalia.

Katika tikio hilo, Agnes Yared (34) mkewe Michael na watoto wake Ezra (8), Witness (6) na Ephraim Michael (3) walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma.

Tukio la tatu lilitokea Septemba 6, 2024 katika Mtaa wa Muungano A uliopo Kata ya Mkonze, ambako Mwamvita Mwakibasi (33) na mwanaye Salma Ramadhani (13) walifanyiwa vitendo vya kikatili na kuwaua.

Inadaiwa katika tukio hilo, watuhumiwa walitumia ngazi kupanda ukuta wa nyumba sehemu ya barazani kisha kushukia katika kochi kwa kutumia kamba.

Pia, watuhumiwa wanadaiwa kuwaua mabinti watatu na kuwachoma moto huku mama mwenye nyumba, Lusajo Mwasonge (40), akijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Tukio hilo lililotokea Mtaa wa Segu Bwawani, Kata ya Nala, jijini Dodoma Septemba 16, 2024.

Mabinti waliopoteza maisha ni mfanyakazi wa ndani Makiwa Abdallah (16), mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Chilohoni, Milcah Robert (12) na Fatuma Mohamed (20).

Fatuma ambaye ni mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma alipatwa na mkasa huo alipokwenda katika sherehe za mahafali ya Milcah.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts