Wananchi Mbeya walia na ubovu wa barabara

Mbeya. Wakazi wa vijiji vya Mwela na Shango Wilaya ya Mbeya wamelalamikia ubovu wa miundombinu barabara kuwa chanzo cha kukwamisha shughuli za kiuchumi na baadhi ya wajawazito kujifungulia njiani.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 22 kutoka Isyonje Wilaya ya Mbeya kwenda Kikondo Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe,  ni tegemeo kubwa kwa wananchi kufuata huduma za afya na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi.

Kilio cha ubovu wa miundombinu hiyo  kimewasilishwa jana Ijumaa Septemba 27, 2924  na wananchi wa vijiji hivyo kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza ambaye anafanya  ziara ya kijiji kwa kijiji.

“Mbunge barabara hii ni kiungo muhimu, lakini imekuwa mbovu kiasi kwamba msimu wa mvua haipitiki na kusababisha wanawake wajawazito kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha yao na watoto wanaojifungua,” amesema Recho Fredy.

Recho amesema ujio wa mbunge wao huenda ikawa suluhisho la kuiomba Serikali kuiboresha kwa kiwango cha lami kabla ya msimu wa mvua kuanza.

“Tunakuwa kama hatupo Tanzania. Barabara hii imekuwa ikitolewa ahadi itafanyiwa maboresho lakini hakuna kinachoendelea, sasa tunaomba tuwasilishie kilio chetu kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuokoa maisha ya wajawazito na kuchochea shughuli za kiuchumi,” amesema.

Naye Alice Mwampashi mkazi wa kijiji cha Mwela amesema licha ya Serikali kusogeza huduma muhimu,  bado wana uhitaji wa kituo cha afya na huduma ya nishati ya umeme kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa.

“Wananchi wa vijiji vya Mwela, Shango na Kimondo tunatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya tunaomba Serikali isikie kilio chetu sambamba na kufikishia huduma ya nishati ya umeme,” amesema.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi, Kaimu Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mhandisi, Kamokene Sanke amesema wanatambua changamoto ya miundombinu ya barabara hiyo na kwamba wataharakisha kuifanyia maboresho

“Kwa kutambua umuhimu wa kipande cha barabara ya Isyonjo- Kikondo wiki ijayo tutaleta makandarasi wawili kuwaonyesha eneo la mradi kwa ajili ya hatua za haraka za kufunga mitambo tayari kwa kuanza kazi,” amesema.

Akijibu kero za wananchi Mbunge  Njeza amewaeleza lengo la ziara yake kijiji kwa kijiji ni kusikiliza changamoto za afya, nishati ya umeme, maji na barabara na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema kuhusu barabara ya Isyonge – Kikondo tayari ilishaombewa bajeti serikalini ya kujengwa kwa kiwango cha lami, huku akibainisha changamoto ilikuwa kwa mkandarasi wa awali aliyepewa zabuni.

“Niwaondoe hofu wananchi barabara hii yenye urefu wa kilometa 22 kutoka Isyonge Wilaya ya Mbeya kwenda -Kikondo Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe, iko mbioni kujengwa kwa kiwango cha lami itakuwa kiungo kikubwa cha shughuli za kiuchumi,” amesema.

Related Posts