Wafurika kuaga miili ya mama, mwana waliofariki kwa kuchomwa moto

Moshi. Mamia ya waombolezaji katika Kijiji cha Marin’ga, mkoani Kilimanjaro wamefurika kuaga miili ya watu wawili kati ya watatu, akiwemo mama na mwanawe  waliofariki dunia kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana na kisha kuitelekeza miili hiyo eneo la msitu wa Hifadhi Korogwe Fuel, uliopo kijiji cha Sindeni wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Jonais Shao (46) ambaye ni mkaguzi wa hesabu za ndani katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na mwanawee Deidan Shao (7) pamoja msichana wao ndani, walichomwa moto usiku wa  Septemba 23, mwaka huu.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye mazishi ya mama na mwanawe waliofariki kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana na kisha kuitelekeza eneo la msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel, uliopo Kijiji cha Sindeni, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga. Picha na Omben Daniel

Vilio na simanzi vimetawala wakati miili hiyo ikiagwa nyumbani kwao, katika kijiji Cha Marin’ga huku baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakishindwa kujizuia.

Miili hiyo inatarajiwa kuzikwa kwenye makaburi ya familia jioni ya leo mara baada ya kumalizika ibada ya mazishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga,  Almachius Mchunguzi  miili ya watu hao ilikutwa imechomwa moto na watu wasiojulikana, usiku wa saa tatu,  Septemba 23, mwaka huu  eneo la msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel.

Kamanda Muchunguzi amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuwatafuta wa husika wa tukio hilo.

Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii kwa taarifa zaidi.

Related Posts