KIPIGO cha mabao 3-1, ilichokipata Kagera Sugar juzi dhidi ya Fountain Gate kimemuweka pabaya kocha mkuu wa kikosi hicho Mganda Paul Nkata ambaye ametakiwa kuandika maelezo kwa viongozi kutokana na mwenendo wa timu hiyo hadi sasa kabla mengine hayajafanyika dhidi yake.
Kichapo hicho ni cha tatu kwa timu hiyo msimu huu kati ya michezo mitano iliyocheza baada ya kushinda mmoja na kutoka sare mmoja.
“Baada ya mchezo wetu aliitwa na viongozi na kupewa taarifa ya kueleza sababu kubwa inayochangia mwenendo mbaya wa timu. Aliporudi kwetu alitugusia suala hilo na kututaka tubadilike sana ili kuokoa kibarua chake,” amesema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
Nkata akizungumzia kiwango cha timu hiyo amesema kuna muda wanakosa bahati ya matokeo mazuri kwa sababu wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga ambazo wanashindwa kuzitumia huku akiweka wazi hahofii kibarua chake kikosini humo.
“Ni ngumu kukabiliana na hali hii kama kocha, kuna wakati unaona wachezaji wanashindwa kutimiza maelekezo unayowapa au kile unachokizungumza labda hawakielewi, inasikitisha lakini tuna nafasi kubwa pia ya kurekebisha kasoro zetu zilizopo.”
Timu hiyo ilianza Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kupoteza michezo miwili mfululizo ikianza na kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, ikachapwa 1-0 na Tabora United, ikatoka suluhu na JKT Tanzania kisha kuifunga KenGold 2-0.
Kichapo cha juzi mbele ya Fountain Gate kinakuwa cha tatu msimu huu kwa Nkata ambaye alijiunga na Kagera Sugar msimu huu akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’, huku akipita timu mbalimbali zikiwemo, SC Villa na Express FC za kwao Uganda.