Mbeya. Licha ya kutangulia kupata bao hadi mapumziko, Ken Gold imeshindwa tena kutamba nyumbani baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa katika Uwanja wa sokoine mjini Mbeya, leo.
Hiyo inakuwa pointi moja ya kwanza kwa timu hiyo ngeni katika michuano hiyo kufuatia vipigo kwenye michezo mitano iliyocheza bila kuonja ushindi wala sare.
Mechi ilizopoteza ni dhidi ya Singida Black Stars ikilala 3-1, ikafa 2-1 dhidi ya Fountain Gate matokeo sawa na Kagera Sugar kisha kudundwa 1-0 na Yanga.
Hata hivyo, Tabora United hawakuwa wanyonge kufuatia upinzani waliouonyesha kupitia kwa supastaa Yacouba Sogne ambaye lhata hivyo nafasi alizopata ameshindwa kuzitumia vyema kutokana na kukutana na ukuta mzito na kushindwa kuupenya jambo liliwafanya kwenda mapumziko wakitanguliwa kwa bao hilo.
Kipindi cha pili, Tabora United wamefanya mabadiliko akipumzika kiungo wa zamani wa Simba, Toto Africans na Kagera Sugar, Abdalah Seseme na kuingia Heritier Makambo dakika ya 46 na kuonekana kubadili mchezo.
Dakika ya 82, timu hiyo ya mjini Tabora iliyotoka kupoteza mechi yake nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya Fountain Gate ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Andy Bikoko.
Matokeo hayo yanaifanya Ken Gold kubaki mkiani kwa pointi moja, huku Tabora United wakifikisha nane baada ya timu zote kucheza michezo sita.
Kocha Mkuu wa Ken Gold, Jumanne Challe amesema licha ya makosa yaliyoonekana tena upande wa mabeki wake, lakini pointi moja waliyoipata siyo mbaya na ndio mwanzo wao wa kusaka ushindi.
Amesema mbali na eneo la beki kuwa tatizo, lakini pia uchovu wa vijana wake baada ya mchezo mgumu dhidi ya Yanga umechangia kukosa pointi tatu nyumbani.
“Beki imerudia makosa yaleyale kuruhusu mpinzani kupiga mpira wa kichwa akiwa huru, japokuwa hata uchovu wa juzi mchezo na Yanga imechangia pia kukosa ushindi kwa leo,” amesema Challe.
“Tunakwenda kujisahihisha makosa yetu kuhakikisha mechi na JKT Tanzania tunapata ushindi. Hii pointi moja ndio mwanzo wa kusaka ushindi, hatujakata tamaa.”
Kocha mkuu wa Tabora United, Francis Kimanzi amesema baada ya kutangulia kufungwa bao, aliamua kufanya mabadiliko kumtoa kiungo mkabaji na kumuingiza straika ili kubadili mchezo.
“Ni kweli nilimpumzisha Seseme na kumuingiza Makambo kwa sababu niliona tumezuia, lakini tumefungwa nikaamua kuongeza nguvu mbele na mipango ikatiki. Pointi moja ya ugenini siyo mbaya,” amesema kocha huyo.
“Tuliwaheshimu wapinzani na sasa tunaenda tena ugenini kuwakabili Dodoma Jiji na tutajipanga kadri tuwezavyo kuweza kupata matokeo mazuri.”